×

Mwigulu Aagiza Ufanyike Uchunguzi wa Kushuka Kwa Bei ya Miwa

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Bodi ya Sukari Tanzania itume timu ya wataalamu kuchunguza sababu za kushuka kwa bei ya miwa inayouzwa na wakulima wa Mikumi, mkoani Morogoro.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumatatu, Novemba 23, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Mikumi Day, Mji Mdogo wa Mikumi, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, kufuatia malalamiko ya wakulima kuhusu bei hiyo na madai ya kuwapo kwa vitendo visivyo vya uaminifu katika biashara ya zao hilo.

Amesema anatambua kuwa bei ya miwa inaweza kupanda au kushuka kutokana na mwenendo wa soko, lakini wakati mwingine mabadiliko hayo yanaweza kuchangiwa na vitendo visivyo vya uaminifu. “Wakati mwingine ni soko, lakini wakati mwingine huwa zinakuwepo na janja janja. Na hata sasa nimegusiwa kwamba zipo na janja janja,” amesema.

Waziri Mkuu ameiagiza Bodi ya Sukari, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, kutuma wataalamu watakaokutana na vyama vya ushirika na wakulima ili kubaini chanzo halisi cha tatizo hilo. “Sasa nielekeze Bodi ya Sukari itume wataalamu waje waonane na vyama vya ushirika pamoja na nyinyi wenyewe wakulima, ili tujue mzizi hasa wa tatizo,” amesema.

Aidha, ameagiza taarifa ya uchunguzi huo iwasilishwe kwake moja kwa moja ili aweze kutoa maelekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhakikisha wakulima wananufaika na shughuli zao za uzalishaji.

“Na taarifa hiyo niipate mwenyewe ili niweze kuelekeza hatua stahiki za kuchukua, ili tuweze kuhakikisha jasho la wakulima wa miwa linapata faida kutokana na nguvu anayowekeza katika kulima,” amesema.

Leave a Comment