
MTANGAZAJI mkongwe wa redio na mshereheshaji wa matamasha nchini Tanzania, Eddo Bashir Sanga, maarufu kwa majina ya Edo Mnyama na Edo Tiger Mnyama, amefariki dunia Novemba 24, 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Consolata Ikonda, iliyopo Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe.
Kifo cha marehemu kimeibua majonzi miongoni mwa watu mbalimbali, wakiwemo wadau wa tasnia ya habari na burudani, kutokana na mchango wake katika tasnia hiyo nchini.
Akitoa salamu za rambirambi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert John Chalamila, ameeleza namna alivyoguswa na taarifa za kifo cha marehemu, huku akifichua mazungumzo yao ya mwisho yaliyofanyika wakati Eddo akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.

Chalamila amesema alipomtumia ujumbe marehemu kumuuliza hali yake, Eddo alimjibu kwa maneno yaliyomgusa sana akisema: “Safari hii sichomoi, niamini Chalamila.”
Amesema kauli hiyo ilimuumiza kisaikolojia, lakini alijitahidi kumtia moyo kwa kumwambia kuwa mwanaume hakati tamaa hadi dakika ya mwisho na kumhakikishia kuwa atapona.
Aidha, Chalamila amemshukuru Salvatori Ngerera kwa kuendelea kumpa taarifa kuhusu maendeleo ya hali ya marehemu katika kipindi chote cha matibabu yake.
Ameeleza kuwa katika mazungumzo yao ya mwisho, Eddo alimtumia ujumbe wa shukrani na kumweleza kuwa angempa mrejesho kuhusu hali yake baada ya mazungumzo yao marefu.

Hata hivyo, amesema kwa masikitiko makubwa kuwa mrejesho wa mwisho alioupokea haukuwa taarifa ya kuimarika kwa afya yake, bali taarifa za kifo chake.
“Jitihada haziwezi kuzidi kudra ya Mungu,” amesema Chalamila, akieleza namna alivyopokea kwa unyenyekevu mapenzi ya Mungu.
Akihitimisha salamu zake, Chalamila amesema atayahifadhi maneno ya mwisho ya marehemu kama kumbukumbu ya pekee, huku akimuombea apumzike kwa amani katika rehema za Mungu.
“Ndugu yangu, tangulia, ukawasalimie wote tuliowapenda waliotangulia mbele ya haki. Tunakuombea upumzike katika rehema za Mungu, na mwanga wa milele ukuangazie,” ameandika Chalamila.
Marehemu Eddo Bashir Sanga anakumbukwa kwa mchango wake katika utangazaji wa redio na uendeshaji wa matamasha mbalimbali nchini Tanzania.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
