×

Tanzania Kutumia Afcon 2027 Kutangaza Utalii Wake Duniani

Tanzania imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa lengo la kutumia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON PAMOJA 2027) kutangaza vivutio vya utalii, utamaduni na ukarimu wa Watanzania kwa mataifa mbalimbali duniani.

Ushirikiano huo umewekwa rasmi kupitia utiaji saini wa mkataba kati ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na CAF, utakaowezesha kutumia jukwaa kubwa la soka la Afrika kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo muhimu ya utalii barani Afrika.

Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Dkt. Theresa Mugobi, pamoja na Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adamu, mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji.

Hafla hiyo imefanyika Jumatano, Novemba 25, 2026, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Fainali za AFCON 2027.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inalenga kutumia mwamko na ufuatiliaji mkubwa wa mashindano hayo kufikisha ujumbe wa utalii wake kwa mamilioni ya mashabiki wa soka kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mkakati huo unalenga kuonesha utajiri wa vivutio vya utalii nchini, ikiwemo hifadhi za wanyamapori, mandhari ya asili, maeneo ya kihistoria, urithi wa kitamaduni pamoja na ukarimu wa wananchi.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa matatu ya Afrika Mashariki yatakayokuwa mwenyeji wa AFCON 2027, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, katika mashindano yanayokwenda kwa jina la AFCON PAMOJA 2027.

Kupitia nafasi hiyo, mataifa hayo yanatarajia kutumia mashindano hayo si kwa ajili ya kuonesha uwezo wa soka pekee, bali pia kutangaza fursa za kiuchumi, utalii na utamaduni wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Ushirikiano kati ya TTB na CAF unaifanya AFCON 2027 kuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania kuunganisha michezo na utalii, huku ukilenga kuongeza mwonekano wa nchi kimataifa na kuvutia wageni zaidi kupitia nguvu ya soka la Afrika.

Leave a Comment