
Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Umma, Renatus Mgusii (katikati) akizungumza jambo mbele ya waandishi wa habari. Pembeni ni baadhi ya viongozi wa tume hiyo.

Waandishi wa habari wakichukua matukio katika hafla hiyo.
TUME ya Utumishi wa Umma imefafanua rufaa za watumishi wa umma na njia wanazopaswa kufuata katika wakati wakiwa na matatizo mbalimbali kazini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Msaidizi wa tume hiyo, Renatus Mgusii, alisema kuwa tume hiyo ni mamlaka ya rufaa katika utumishi wa umma, hivyo hupokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma wanapopinga uamuzi wa Mamlaka za Nidhamu kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1)b cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na 8 ya mwaka 2002 na kanuni ya 61 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.
Amesema mamlaka zingine za rufaa ni Rais ambaye ni mamlaka ya rufaa kwa watumishi wote ambao mamlaka yao ya nidhamu ni Katibu Mkuu Kiongozi.
Vilevile alisema Rais ni mamlaka ya rufaa kwa watumishi wa umma wote na mamlaka za nidhamu ambazo hazikuridhika na uamuzi wa tume ambapo uamuzi wake ni wa mwisho katika mkondo wa kiutawala.
Aidha alieleza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2015/16 tume ilipokea rufaa 66 kutoka kwa watumishi na kati ya hizo 36 zilikataliwa lakini 10 zilikubaliwa kwa masharti kutokana na tume hiyo kukubaliana na adhabu walizopewa warufani kwamba walistahili adhabu hizo.