×

Mwinyi Kuongoza Matembezi Wiki ya Sheria Dar

sheria-1

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizungumza na wanahabari.  Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakam Kuu Tanzania Jaji Ferdinand Wambali

sheria-2

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Katarina Revocati (wa kwanza kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo.

sheria-3

Viongozi meza kuu wakisikiliza kwa makini maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabari (hawapo pichani).

NA DENIS MTIMA/GPL

RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, anatarajiwa kuongoza matembezi ya Wiki ya Sheria kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi  viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Januari 29 mwaka huu  ambapo kilele cha wiki hiyo  kinatarajiwa kufanyika Februari 2  katika viwanja vya mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar.  Mgeni rasmi katika hafla hiyo atakuwa Rais John Magufuli.

Katika matembezi hayo Mwinyi atazindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Sheria ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuelekea maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini ambapo pia katika mikoa yote ya Tanzania wananchi wataweza kupata fursa ya kujua sheria katika sehemu maalum zitakazokuwa zimeandaliwa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania  Prof. Ibrahim Hamis Juma,  amesema mahakama itawaelimisha wananchi jitihada mbalimbali ilizochukua zenye lengo la kuboresha huduma zake kupitia mpango-mkakati wa miaka mitano inaoutekeleza katika kutoa haki kwa wakati na kuwezesha ukuaji wa uchumi.  Haya yatafanyika kwenye mabanda yatakayokuwepo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja kabla ya kilele chake.

Jaji Juma ametoa rai kwa wananchi kutembelea sehemu zote zilizoandaliwa kwa ajili ya utoaji elimu ya sheria nchini kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali na kupata huduma  za kisheria

Miongoni mwa  huduma zitakazotolewa katika wiki hiyo  ni pamoja na taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi mbalimbali za mahakama, taratibu za kesi za dhamana, taratibu za rufaa,  taratibu za kesi za mirathi, ndoa na talaka, taratibu za kupokea na kushughulikia malalamiko na msaada wa kisheria.

Maadhimisho ya siku hiyo nchini mwaka huu yanakuja na kaulimbiu ya:  ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati; Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi’.

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam