×

Umejifunza Nini Baada ya Kupata Mpenzi Sahihi?

black-dating-loving-couple-480Na Boniphace Ngumije| CHAMPIONI JUMAMOSI

NI jambo jema kumshukuru  Mungu kila tuamkapo, tutembeapo na tuwapo katika shughuli zetu mbalimbali za kila siku. Mpenzi msomaji wangu ni vizuri kutambua kuwa ni neema ya pekee mimi na wewe kukutana hapa leo na sina budi kukukaribisha katika mada ya leo ambayo inakuuliza wewe; Umejifunza nini baada ya kumpata mpenzi sahihi?

Nafahamu inaweza kukushitua kidogo. Ukajiuliza nini ujifunze wakati umekwisha mpata mpenzi ambaye ni sahihi kwako yaani ‘wife material’. Unaweza hata kujiambia;

“Hapa nimemaliza” “nitulie sasa, nifanye maisha na mambo yangu mengine ya maendeleo.” Ni kweli kabisa, hivyo ndivyo inatakiwa kuwa, lakini katika safari ya kumpata huyo mpenzi wako umejifunza nini? Je, umejifunza ni kazi rahisi kumpata mpenzi sahihi maishani?

Au ni kazi ngumu?

Je, umejifunza ni mpango wa Mungu kumpata mpenzi sahihi au jitihada binafsi?

Au umejifunza kuwa mpenzi sahihi anakuja mwenyewe katika maisha ya kila mtu?

Ukweli ni kwamba kuna mambo mengi sana ya kujiuliza na kujifunza pale unapopata mwanamke au mwanamme sahihi kwako zaidi ya kubweteka na kuridhika kuwa tayari unaye na wengine kwenda mbali zaidi kwa kuanza kuwatesa, kuwanyanyasa na kuwasumbua wapenzi wao kwa sababu tu wanakuwa na mapenzi ya dhati kwao.

Ngoja nikwambie kitu ndugu yangu, unapaswa kutambua kuwa kumpata mwenza wa kweli pamoja na mambo yote ya kiimani na mazingira ni kazi ngumu sana. Hilo ndilo kubwa ambalo mtu yeyote mwenye akili timamu anatakiwa kulifahamu ili kujua ni jinsi gani atamtunza na kuishi na mpenzi wake huyo kwenye maisha yenu yote.

 Lakini usipofahamu ni rahisi kumtenda na kutomtunza jambo ambalo linaweza kusababisha akaondoka, baadaye ukajilaumu na kujutia hasa pale utakaposhindwa kumpata mpenzi mwingine ambaye atakuwa sahihi kwako.

Watu wengi wamejikuta wakilia na kusaga meno kwa makosa madogo sana waliyoyafanya kwenye maisha yao ya kimapenzi, walilia na kulia walipokuwa kwenye uhusiano na watu wasiyo sahihi ajabu ni kwamba hata walipopata wenza sahihi bado watu hao waliendelea kulia!

Napenda msomaji wangu utambue misingi na adabu kwenye maisha ya uhusiano, ukweli ni kwamba unaweza kuwa umepata mtu sahihi lakini wewe usiwe sahihi kwake, kama hutosimama kwenye misingi sahihi ni wazi utaendelea kulia wakati wote.

Ni ukweli usiopingika kuwa misingi ya penzi sahihi inajengwa kwa kusikilizana, kupendana na kuheshimiana. Kila wakati binadamu tunatakiwa kujifunza mambo mapya kwenye maisha, kujifunza huko ndiko kunapotupa fikra pana katika maisha yetu ya kila siku, kukuhoji umejifunza nini baada ya kupata mpenzi sahihi, lengo ni kutaka kukumbusha kuwa bado upo kwenye safari isiyokuwa na mwisho, safari ya kuendelea kujifunza na kubaini mambo mapya ambayo yanaweza kukusaidia kwenye maisha yako ya kila siku hasa ya kiuhusiano.

Mara kadhaa nimekuwa nik ipokea malalamiko mengi kutoka kwa wasomaji kadha wa kadha, wamekuwa wakilalamika kuwa ingawa wapo kwenye uhusiano na watu ambao wanaona ni wenza sahihi lakini wamekuwa hawana furaha kwenye maisha yao.

Nilichobaini katika maelezo yao kulingana na kesi husika, kwa ujumla niliona kuna tatizo la kutojifunza baadhi ya mambo sanjari na uzembe mdogo kwenye baadhi ya maeneo, kujifunza ni kitu kimoja na kuelewa ulichojifunza na kukifanyia kazi ni jambo jingine.

Pamoja na kwamba penzi la kweli linajengwa kwenye misingi ya kupendana, kuheshimiana na kusikilizana lakini ukweli ni kwamba hakuna uhusiano wa kweli  usiokuwa na changamoto ya migogoro ya hapa na pale. Jifunze kupenda kwa dhati, kumuheshimu na kumsikiliza mpenzi wako, ili nawe uwe mtu sahihi kwake, jifunze kulingana na makosa uliyoyafanya au kufanyiwa kabla ya kuwa na mtu huyo.

Kwa leo ni hayo tu, tukutane siku nyingine kwa mada nyingine.

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam

Save