The House of Favourite Newspapers

Sakata la Unga… Watuhumiwa Wapewa Dhamana na Masharti Matatu Mahakamani

 

Wafanyabiashara, wasanii wa muziki na filamu wakiwa chini ya ulinzi wajeshi la polisi

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam imewaachia kwa dhamana wasanii 13 katika tuhuma za kutumia dawa za kulevya, huku wakiwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi.

Khalid Muhammed T.I.D akiwa chini ya ulinzi

Mapema leo katika mahakama hiyo, palitawaliwa na idadi kubwa ya watu wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki waliofika tangu asubuhi kwa ajili ya kushuhudia ndugu zao wanavyofikishwa mahakamani hapo.

Hata hivyo, baadhi ya watu walisikika wakilalamika kutokana na kutomuona aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006 na muigizaji wa filamu, Wema Sepetu  Sepetu.

Wasanii hao  waligawanywa kwenye makundi mawili ambapo la kwanza lilikuwa na wasanii wanane wakitetewa na Wakili Albert Msando, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kundi la pili lilikuwa na wasanii wanne kisha kupandishwa kizimbani kwa hakimu mwingine.

Katika kundi la kwanza lilijumuisha wafuatao;   Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu), Rajabu Salum, Romeo Bangura (Romijous), Cedou Madigo, Khalid Mohammed (T.I.D), Johana Mathysen, Rechoel Josephat (Recho Kizunguzungu) na Anna Kimaro (Tunda).

Akizungumza katika kesi hiyo inayowakabili, Wakili wa Serikali Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Huruma Shaidi, alidai kuwa upande wa Jamhuri unawasilisha maombi yenye vipengele vitatu chini ya kifungu cha 73 (e) na 74 cha sheria ya makosa ya jinai.

Alieleza kuwa katika maombi hayo matatu yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Ofisa Mkuu Msimamizi wa Kitengo cha Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya wa Kituo Kikuu cha Kati, Denis Mujumba.

Wakisubiri kuingia mahakamani

Alisema kuwa ombi la kwanza ni kuwa mahakama iwaamuru wajibu maombi kuwa na tabia njema wakisimamiwa na wadhamini wao kwa kipindi cha miaka mitatu na kuripoti Kituo cha Polisi cha Kati mara mbili kwa mwezi ili kuangaliwa mwenendo wa tabia zao.

Aidha, maombi ya pili ni kuwa liwe jukumu la mahakama kuangalia itatoa masharti gani yoyote dhidi ya wajibu maombi hao (watuhumiwa).

Wakili Katuga alidai kuwa ndani ya hati ya kiapo cha Denis Mujumba ameeleza kuwa yeye ni askari polisi ambaye pia ni mpelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Dar es Salaam.

Alieleza kuwa wajibu maombi ni wakazi wa Dar es Salaam, hivyo akiwa ni mkuu wa kitengo cha upelelezi ana taarifa za kina kuhusu wajibu maombi hao na wenzake kujihusisha na dawa hizo za kulevya.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa kutokana na tabia hiyo endapo wakiachwa bila kuwa chini ya uangalizi huenda wakasababisha uvunjifu wa amani katika jamii, akaiomba mahakama kupokea hati hiyo ya kiapo ikiwa na maombi hayo.

Naye wakili wa utetezi, Albert Msando alipinga hoja hizo na kuieleza mahakama kuwa  kiapo hicho cha askari upelelezi kina mapungufu kwa kuwa kinawazungumzia wajibu maombi kwa ujumla na bila kueleza ni taarifa zipi, zimepatikana wapi kwa nani na lini.

Alieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia wajibu maombi hayo kujua kwamba wanahusika vipi katika maombi hayo hadi kufikishwa kizimbani na  kuhusu suala la uangalizi alidai kuwa inatambulika kuwa ni kweli dawa za kulevya ni hatari lakini si vyema kwa wajibu maombi hao kuripoti kituo cha polisi kwa mwezi mara mbili ama kuwa chini ya uangalizi kwani hilo ni jukumu la jeshi la polisi.

Baada ya kuwepo kwa mvutano huo, Hakimu Shaidi alitoa uamuzi wake na kusema kuwa wajibu maombi hao watakuwa chini ya uangalizi chini ya mwaka mmoja  kifungu cha 73 (e) na 74 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na kujidhamini wenyewe kwa dhamana ya Sh. milioni 10 kila mmoja pamoja na kuripoti kituo cha kati cha polisi kwa mwezi mara mbili.

Kwa upande wa kesi nyingine ya wajibu maombi ambao ni Ahmed Hashim (Petiti man), Nassor Nassoro, Bakari Mohamed na Lulu Chelangwa (Luludiva), Said Masoud (Said Alteza) walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha chini ya wakili wa serikali, Nassoro Katuga akishirikiana na Elia Athanas alidai kuwa upande wa Jamhuri umewasilisha maombi  chini ya kifungu 73 (e) cha mwenendo wa makosa ya Jinai.

Wakiingia mahakamani

Akizungumza katika kesi hiyo wakili Katuga aliyaeleza maombi hayo ambayo awali aliyasoma kwa Hakimu Huruma Shaidi wakati kundi la wasanii wanane walipopandishwa kizimbani.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Wakili Msando alieleza kuwa wanakubaliana na maombi ya upande wa Jamhuri, isipokuwa wanapinga suala la wajibu maombi kuripoti Kituo cha Polisi cha Kati.

Katika uamuzi wake Hakimu Mkeha alisema kuwa mahakama hiyo imeyapokea maombi hayo ya Jamhuri na kukubaliana nayo.

Alisema kutokana na maombi hayo yalivyowasilishwa, wajibu maombi hao watakuwa chini ya uangalizi kwa miaka mitatu, pia wataripoti kwenye Kituo cha Polisi cha Kati mara mbili kwa mwezi pamoja na kujidhamini wenyewe kwa dhamana ya Sh. milioni 20 pamoja na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana hiyo.

NA MUSA MATEJA | GLOBAL PUBLISHERS

Sakata la Unga; Watuhumiwa Wapewa Dhamana na Masharti Matatu Mahakamani

Comments are closed.