
Na GABRIEL NG`OSHA| GAZETI LA AMANI| SHOWBIZ XTRA
MUZIKI ili ukamilike unahitaji mtunzi, mtayarishaji, muimbaji na wengineo. Watayarishaji na watunzi wengi wa Kibongo hawapewi nafasi kwenye baadhi ya nyimbo ambazo wamehusika licha ya nyimbo hizo kufanya vyema kwenye gemu.

Showbiz Xtra imefanikiwa kuzungumza na mtunzi na mwimbaji wa nyimbo na baadhi ya viitikio vya nyimbo za mastaa, Juma Ramadhani ‘Chin Bees’ anayefanya vizuri na wimbo wake wa Zuzu:
Showbiz Xtra: Una mchango mkubwa sana kwenye nyimbo za Kibongo lakini hufahamiki, hii imekuaje?
Chin Bees: Kiukweli sijui inakuaje lakini naamini hata kama ukibaniwa vipi muda ukifika hakuna anayeweza bana.
Showbiz Xtra: Ni nyimbo zipi ambazo umewahi kuhusika kwa sana na zikafanya vizuri?
Chin Bees: Ni nyingi ambazo nimeshiriki katika kuimba kwenye viitikio kama Sweet Mangi ya Nikki wa Pili, Alosto ya G. Nako, Mwendokasi ya Quick Rocka na nyingine kibao.
Showbiz Xtra: Inasemekana wewe pia ni mtunzi, umeandika nyimbo ngapi hadi sasa?
Chin Bees: Nimeandika nyimbo nyingi, nazo ni Never Ever ya Vanessa Mdee, Kamatia Chini ya Kundi la Navy Kenzo na Nipendelee.
Showbiz Xtra: Mbona hujulikani, husikiki hata kupewa sharauti kwenye kazi zako?

Chin Bees: Nyuma ya gemu na mafanikio kuna mambo mengi sana, ingawa nyimbo zingine nilitegemea iwe hivyo lakini nikabaniwa.
Showbiz Xtra: Kwani huwa unalipwa katika kutunga au kuimba kwenye nyimbo za mastaa?
Chin Bees: Hapana sijawahi kulipwa, zingine zinakuwa ni nyimbo za studio kwa hiyo nilifanya tu ila ilitegemea nipewe shavu hata kwa kutajwa lakini siyo wote waliofanya hivyo.
Showbiz Xtra: Hadi sasa una nyimbo zako ngapi ulizoimba?
Chin Bees: Nina nyimbo zangu ambazo zimeishatoka na kuniweka kwenye ramani kama vile Ruba, Niko Mbali, Zuzu pamoja na Pepeta ambayo nitaiachia Ijumaa, (kesho).
Showbiz Xtra: Kazi zako unasimamiwa na nani?
Chin Bees: Niko chini ya uongozi mzuri wa Mkurugenzi Dash wa Kampuni ya Wanene Entertainment, naamini nitafanya kazi kali na nzuri zenye ubora za levo ya kimataifa.