×

Kesi ya Mbowe Vs RC Makonda, Sirro na Kamanda Wambura Yaanza Kuunguruma Mahakama Kuu

DAR ES SALAAM: Kesi ya kupinga kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Jeshi la Polisi Dar, Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Camilius Wambura imeanza kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, Mbowe anapinga kukamatwa na Jeshi la Polisi Dar kufuatia wito wa RC Makonda aliyemtaja kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya na kumtaka aende katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar pamoja na watuhumiwa wengine 65 kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Katika kesi hiyo,  mbali na mambo mengine, Mbowe anapinga amri ya Makonda ya kutaka akamatwe na pia kile alichokiita kudhalilisha watu wakati mkuu huyo wa mkoa alipotaja majina ya watu.

Kesi hiyo imanza kunguruma leo huku Mahakama ikiwaagiza mawakili wawili wa upande wa utetetzi (upande wa Mbowe) kufanya mabadiliko katika baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye kesi yao ya msingi iliyowasilishwa mahakamani hapo kabla ya Machi 8, mwaka huu.

Hata hivyo, Wakili wa Mbowe, Peter Kibatala vipengele hivyo watavirekebisha na kuviwasilisha kabla ya mahakama kufungwa leo hii hii.

Katika hatua nyingine, leo Mwanasheria nguli Tanzania Generali Ulimwengu ametinga mahakamani  hapo akiwa kama wakili wa Freeman Mbowe kwenye kesi hiyo na kuibua maswali miongoni mwa watu waliokuwepo mahakani hapo kufuatilia kesi hiyo.

Mnamo Februari 21, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitupilia mbali ombi la Jeshi la Polisi la kutaka kumkamata Freeman Mbowe na kukubali maombi ya mawakili wa Mbowe kwamba asikamatwe hadi kesi itakaposikilizwa tena.