Na Mwandishi wetu |CHAMPIONI| Dar es Salaam
STRAIKA supastaa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, juzi aliwaambia wachezaji wa Tanzania kuwa wanapopata nafasi ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa Ulaya, basi wahakikishe wanazitumia vizuri nafasi hizo kwani ni adimu.
Samatta amekuwa mchezaji mwenye mafanikio makubwa, akiipeperusha vyema bendera ya Tanzania, kwani ameendelea kuwatesa Wazungu kwa ufundi wake mwingi anaoumiliki miguuni m wake.
Championi tunaamini alichokisema Samatta ni somo zuri kwa wachezaji wetu kwani wengi wao wamekuwa wakipata nafasi nyingi za majaribio lakini wanashindwa kuzitumia vizuri au wanazitumia vyema lakini baada ya muda wanarudi Bongo kwa kushindwa kuonyesha kiwango nje ya nchi.
Tumewashuhudia wachezaji wengi wakirudi Bongo baada ya kushindwa kucheza Afrika Kusini, Ulaya na kwingineko. Samatta alisema tatizo kubwa ni nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.
Tunaungana na Samatta kuwashauri wachezaji wengine kuwa wanapopata nafasi ya kwenda kufanya majaribio au kwenda kucheza soka la kulipwa, basi wazitumie vizuri kwani nafasi hizo ni adimu.
Tunaamini tukiwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa kwa kiwango cha juu kwenye klabu kubwa kama ilivyo kwa Samatta, tutapata timu nzuri ya taifa na hatimaye tutaanza kufanya vizuri.