
Na Omary Mdose/CHAMPIONI/GPL
BAADA ya kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao huku ikianza mapema harakati za usajili wa kukijenga kikosi chao, uongozi wa timu ya Singida United umeibuka na kusema kuwa wataendelea kufanya usajili mpaka pale watakapoona pesa zao zimekwisha.
Singida United baada ya kupanda daraja, ilianza kufanya usajili wa kiungo Mzimbabwe, Tafadizwa Kutinyu pamoja na kumchukua Kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm kabla ya wikiendi iliyopita kuwanyakua Wazimbabwe wengine wawili, Elisha Muroiwa na Wisdom Mtasa.
Kutokana na kufanya usajili huo wa maana, wadau mbalimbali wamekuwa wakijiuliza ni wapi timu hiyo inapata pesa za kufanya usajili huo, hali ambayo imemfanya katibu wa klabu hiyo Abdulrahman Sima kutoa ufafanuzi.
“Hii ni kampuni na kama ilivyo kampuni yoyote ile inakuwa na pesa za kutosha za kujiendesha, kwa hiyo watu wasiwe na maswali mengi sana ya kujiuliza jeuri hii ya pesa za usajili tunaipata wapi kwani tunataka kufanya usajili mpaka pesa tulizozitenga ziishe.
“Lakini tumeamua kufanya hivi mapema kwa sababu tunataka kufanya kweli msimu ujao katika ligi, tangu tulipokuwa ligi za chini, malengo yetu yalikuwa ni kufika juu, sasa tumefika na tunataka mafanikio zaidi.
“Kitu cha kwanza tulichojiwekea wakati tunaanza harakati za kupanda ligi kuu ni kufanikisha tunaopanda na kweli imekuwa hivyo, sasa tunataka ubingwa ili tuje tuiwakilishe nchi katika michuano ya kimataifa,” alisema Sima.
Licha ya katibu kutoa kauli hiyo, taarifa zingine zinasema kuwa, timu hiyo imekuwa ikipata jeuri hiyo kutoka kwa matajiri na watu maarufu waliopo kwenye timu hiyo kama mfanyabiashara, Mohammed Dewji na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.