Hans Mloli
SIMBA imeamua kufanya usajili wa kweli kwa ajili ya msimu ujao baada ya kutoka na msimamo wa kusajili maprofesheno wengine wapya sita wanaotumainiwa kuja kufuta ukame wa kombe la Ligi Kuu Bara klabuni hapo.
Imewekwa wazi kuwa kilichopo mezani kwa sasa kuhusiana na usajili wa klabu hiyo ni kusajili mabeki wawili wa kati, viungo wawili na mastraika wawili, wote kutoka nje kisha kumaliza na usajili mdogomdogo wa wachezaji wa ndani.
Ingawa bado sakata la shutuma za utovu wa nidhamu kwa wachezaji wa kimataifa waliopo kwenye timu hiyo halijaisha, lakini taarifa zinaeleza kuwa hakutakuwa na maamuzi mengine zaidi ya kuachana na wachezaji hao kisha nafasi zao kuchukuliwa na majembe hayo sita mapya.
Mrundi, Emiry Nimubona, Mkenya, Paul Kiongera, Waganda, Hamis Kiiza, Juuko Murshid na Brian Majwega wapo nje ya kikosi hicho kwa sasa kutokana na shutuma hizo.
Mchezaji pekee wa kimataifa anayetarajia kubaki kikosini hapo ni kipa Muivory Coast, Vincent Angban pekee kwa kuwa Mzimbabwe, Justice Majabvi imethibitika kuwa hatakuwa na timu hiyo msimu ujao kutokana na masuala ya kikazi ya mkewe.
Tayari imeripotiwa kuwa viungo kutoka Cameroon, Patrick Ghomsi na Outarra Kader na Morisane Sangare raia wa Ivory Coast wameshatajwa kuanza mazungumzo na vigogo hao lakini pia yumo beki kutoka DR Congo ambaye bado hajajulikana jina lake, naye ameelezwa kutazamiwa kutua klabuni hapo.
“Usajili wa ndani upo lakini imepitishwa lazima ufanyike usajili wa nguvu wa wachezaji wapya sita wa kimataifa katika nafasi hizo,” kilisema chanzo cha ndani kutoka timu hiyo na kuongeza:
“Kiiza na Juuko bado wana mikataba lakini wanatafutiwa namna, kama ni kuachana nao kabisa au kuwatoa kwa mkopo maana uongozi haujafurahishwa kabisa na huu utovu wa nidhamu waliouonyesha.
“Kuna beki kutoka Congo naye anaangaliwa na alishakuja nchini mara ya kwanza tukazungumza kidogo na sasa anatarajiwa kuja tena kuangalia tutaafikiana wapi. Lakini na usajili wa ndani utafanyika kwa kiwango kikubwa pia kwa ajili ya kuimarisha zaidi timu,” alimalizia mtoa taarifa huyo.