
Na Mwandishi wetu/CHAMPIONI/GPL
MOJA kati ya viungo bora kwenye soka duniani ni Xabi Alonso, ambaye kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Bayern Munich.
Xabi amefanya kazi kubwa ya kulijenga jina lake kwenye soka duniani kote na sasa anatajwa kama viungo waliofanikiwa sana kwenye ulimwengu huu.
Alonso ambaye ameshazichezea timu kubwa duniani kote na kutwaa makombe kadhaa ya heshima ameshatanagaza kuwa ataachana na soka mwishoni mwa msimu huu.
Kiungo huyo raia wa Hispania, alitumika kwa mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Liverpool kwa miaka mitano, tangu mwaka 2004 na 2009 na kati ya mafanikio makubwa aliyopata ilikuwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mwaka 2005.
Hata hivyo, pamoja na kukiri mara kwa mara kuwa ana mapenzi makubwa na Liverpool aliamua kuondoka kwenye timu hiyo na kujiunga na Real Madrid ambapo pia alipata mafanikio makubwa na sasa amekwenda kumalizia soka lake nchini Ujerumani.
Kwa Ulaya ligi kubwa ni tano, lakini zile ambazo zinaheshimika sana ni tatu, Ligi Kuu England, Premier, Ligi Kuu Hispania, La Liga na ile ya Ujerumani, Bundesliga, jambo ambalo linaonyesha kuwa kiungo huyo anastaafu baada ya kutumika kwenye ligi zote kubwa barani humo.
Alonso anastaafu akiwa na umri wa miaka 35, na hadi mwishoni mwa msimu huu atakuwa ameshacheza soka kwa miaka 18, jambo ambalo siyo dogo kwa mchezaji yeyote duniani.
Hata hivyo, bado ana nafasi kubwa zaidi ya kuendeleza umaarufu wake endapo ataisaidia timu yake ya Ujerumani kutwaa ubingwa wa Bundesliga mwishoni mwa msimu huu kwa sasa wakiwa kileleni na pointi 62 tofauti ya pointi 11 na timu inayoshika nafasi ya pili.
Msimu huu staa huyo mwenye uwezo wa kupiga mashuti makali ameshafanikiwa kufunga mabao mawili, akiwa anapata nafasi kwenye kila mechi ya timu yake ambayo inatafuta ubingwa wa 27 wa Ligi Kuu ya Bundesliga.
Kiungo huyo akiwa na Liverpool alipata mafanikio makubwa sana baada ya kuichezea michezo 210 na kufunga mabao 19, huku mengi akiwa amefunga akiwa nje ya eneo la hatari.
Kwa kipindi chote alichokaa kwenye timu ya Liverpool staa huyo alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Kombe la FA.
Hata hivyo, bado amekuwa akitajwa mara kwa mara kuwa anaweza kurejea tena kwenye timu hiyo kama kocha wa vijana.
“Naipenda sana Liverpool, hii ni timu kubwa kwangu na kila ninapokaa natamani kurejea tena kwenye timu hiyo, hakika hii ni timu bora kwangu na yenye heshima kubwa.
“Hata mtoto wangu amekuwa akiniuliza kwanini haturudi Liverpool, namwambia nipo bize, lakini naamini kuwa hapo ni sehemu ninapopapenda sana.
“Bado nimekuwa nikiwasiliana na watu wengi pale Liverpool, nina marafiki na watu wengine muhimu sana ambao tumekuwa wote kwa kipindi kirefu,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Hispania.
Kiungo huyo ambaye alianzia soka lake kwenye kikosi cha Real Sociedad akaenda Eibar ameshacheza michezo 691 na kufunga mabao 44 kwenye klabu zote nne alizozitumikia.
Kwenye timu ya taifa ambayo ameichezea tangu mwaka 2002, kiungo huyo ambaye alitwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2010, pamoja na Kombe la Euro mwaka 2008 na 2012, ameshatumika kwenye timu hiyo katika michezo 114 na kufunga mabao 16.