×

TRA Yakomaa, Simba Yazikomboa Nyasi

Wilbert Molandi | CHAMPIONI| Dar es Salaam

NYASI bandia za Simba zipo hatarini kupigwa mnada na Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart, baada ya uongozi wa timu hiyo kushindwa kuzilipia ushuru wa dola 40,000 (zaidi ya shilingi milioni 87).

Nyasi hizo, zilifika kwenye bandari ya Dar tangu Oktoba, mwaka jana maalum kwa ajili ya kuziweka kwenye uwanja wao mpya wanaoujenga Bunju jijini Dar.

Kampuni hiyo ya mnada jana asubuhi ilitangaza mnada huo baada ya nyasi hizo na magoli ya klabu hiyo kukaa bandarini kwa muda wa miezi sita tangu zifike, ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndiyo ambayo inasimamia masuala ya ushuru lakini jana jioni ilifahamika kuwa Simba ilikuwa njiani kuzikomboa nyasi hizo.

Taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata ni kuwa mnada huo ulitarajiwa ufanyike nyuma ya The Waterfront Sunset Restaurant and Beach Bar Barabara ya Yatch Club Masaki katika ofisi za LW9, jana.

Mtoa taarifa huyo alisema, nyasi hizo zinapigwa mnada na kampuni hiyo baada ya Simba kushindwa kuzikomboa kwa wakati.

“Mzigo wowote kukaa bandarini mwisho ni miezi sita, kwani ikifikia miezi hiyo mzigo unapigwa mnada na kampuni husika waliyoipa tenda ya kupiga mnada.

“Hivyo, basi Simba mzigo wao umefika tangu Oktoba, mwaka jana na hakuna dalili yoyote ya kuzitoa nyasi hizo bandia, hivyo muda umefika na hakuna budi, zinapigwa mnada,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alikiri kupata taarifa ambazo zimewashtua huku akiahidi kufanya kikao na viongozi wenzake ili kupata fedha.

Simba hivi karibuni iliunda Kamati ya Maendeleo ya Ujenzi wa Uwanja Bunju Complex iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe ikiwa na wajumbe wake Ally Sullu, Adam Mgoyi, Crescentius Magori, Imani Kajula na Jerry Yambi.

Taarifa za uhakika ambazo zilifika kwenye meza ya gazeti hili ni kuwa uongozi wa Simba ulikuwa kwenye mipango ya kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinalipwa na nyasi kukombolewa, hivyo kama hilo lilifanikiwa inamaanisha kufikia leo wanaweza kuwa wamekamilisha dili.