×

Rekodi za Chirwa Noma, Zaibeba Yanga SC

Mwandishi Wetu | CHAMPIONI| Dar es Salaam

TARATIBU Obrey Chirwa anazidi kuwa staa ndani ya Yanga, kwani rekodi zake katika michezo ya hivi karibuni, ndizo zinazoibeba Yanga na juzi alifunga bao pekee lililoiwezesha timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Chirwa alipiga jumla ya pasi 19. Alipiga pia mashuti mawili huku shuti moja likizaa bao alilofunga dakika ya 70.

Kabla ya mchezo wa juzi, Chirwa ambaye ana mabao tisa katika chati ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara, bao lake dhidi ya Toto kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Oktoba 19, mwaka jana, lilichangia timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-0, huku lingine likifungwa na Simon Msuva.

Katika mchezo dhidi ya Kagera Oktoba 22, mwaka jana, alifunga mabao mawili yaliyoiwezesha timu yake kupata ushindi wa mabao 6-2 kwenye Uwanja wa Kaitaba, uwanja ambao jana Simba iliangukia pua. 

Oktoba 26, Chirwa alifunga bao moja na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. Utakumbuka kwamba, mwanzoni mwa mwaka huu, Januari 29, Chirwa alifunga mabao mawili yaliyotosha kuiangamiza Mwadui FC 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

Mechi yake ya mwisho kufunga kabla hajaivaa Azam ilikuwa ni Stand ambapo Yanga ilishinda 4-0. Hata hivyo, vurugu zake zilisaidia Yanga kupata penalti iliyoipa bao moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting Taifa, Machi Mosi. Unaweza ukaona ni jinsi gani anavyoibeba Yanga.

 

Subscribe kwenye YouTube Chanel yetu ya Global TV Online ili zote kali zinazotufikia iwe nisiasa, michezo, comedy, burudani, stori za mastaa, muziki na nyingine zikufikie kwa wakati.