
Na Waandishi Wetu, AMANI | DAR ES SALAAM:
Inatisha! Kufuatia tamko la Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwataka watumishi wa umma walio na vyeti feki kujiondoa wenyewe makazini, Gazeti la Amani lilizunguka kwenye baadhi ya Hospitali za Jiji la Dar na kubaini madaktari, wauguzi na wagonjwa wako kwenye hali mbaya.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, huduma katika Hospitali za Mwananyamala, Amana, Palestina na kwingineko zinatisha kutokana wafanyakazi kujitumbua wenyewe kabla ya Mei 15, mwaka huu kama rais alivyotangaza. Waandishi wetu walifanikiwa kuzungukia katika hospitali hizo ili kubaini ukweli wa madai hayo ambapo hali ilikuwa hivi;
HOSPITALI YA PALESTINA
Kwa upande wa Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza jijini hapa, wagonjwa wengi walikuwa wamekaa, msongamano ulikuwa ni mkubwa, huku baadhi ya milango ya madaktari ikiwa imefungwa kufuli ikiwemo, mlango wa daktari wa macho na daktari wa wazee, ofisi ya mgavi, upande wa mapokezi ambapo huwa kuna vyumba viwili ila kimoja tu ndiyo kilikuwa kikifanya kazi huku kitengo cha dharura kiliendelea kufanya kazi kama kawaida.
Upande wa wodi ya wazazi, msururu wa wagonjwa ulikuwepo huku wengine wakionekana kuchukua usafiri wa Bajaj na kuondoka ingawa haikufahamika kama waliondoka kwa sababu ya kukosa huduma ama la!.
“Ingawa Siku ya Wafanyakazi ‘Mei Mosi’ imechangia lakini kuna wauguzi wengine wamejitumbua wenyewe kuogopa kufikishwa mahakamani,” kilisema chanzo chetu.
Rais Dk. John Pombe Magufuli akipokea ripoti ya watumishi jewa kutoka kwa Waziri wa Utumishi, Angella Kairuki.
MGANGA MKUU PALESTINA
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Palestina, Dk. Kayola Richard alipotafutwa kuzungumzia uala hilo alisema yeye hana mamlaka ya kuzungumza ila alikiri kuwepo walioathirika.
“Kwa sasa siwezi kuzungumzia suala hilo, ni kweli walioathirika wapo ila kuhusu idadi mimi sina mamlaka hayo,” alisema.
HOSPITALI YA AMANA
Wandishi wetu walipofika katika Hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana, ambapo ilifanikiwa kubaini kuwa wafanyakazi kadhaa walikuwa wamejitumbua wenyewe akiwemo daktari mmoja, mfamasia mmoja na manesi wa kuchoma sindano watatu.
Hata hivyo, gazeti hili lilibaini kuwa wengi wa wauguzi hao waliojitumbua ni wale ambao walikuwa ni wahamiaji, ambao hawakuwa na ajira ya moja kwa moja hospitalini hapo.

Waziri Ummy Mwalimu.
HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Kwa upande wa Hospitali ya Mwananyamala ambayo inahudumia wakazi mbalimbali wa Wilaya ya Kinondoni na maeneo mengine ya Dar es Salaam, Gazeti la Amani lilinyetishiwa kuwa kuna wafanyakazi tisa waliokuwa wamejitumbua wenyewe huku wengine wakitarajiwa kuongezeka.
Kutokana na hali hiyo vyanzo vya karibu vilieleza kuwa huduma kwa siku mbili tangu Rais Magufuli awatumbue wafanyakazi hao, imekuwa si nzuri kama ilivyokuwa awali.
“Wapo waliojiengua licha ya kwamba walikuwa ni ‘majembe’, wengi ni wanawake na sekeseke limeikumba theather, wodi ya wazazi,wodi ya watoto na OPD,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutoandikwa gazetini.
MSIKIE MGANGA WA MANISPAA
Gazeti la Amani lilifunga safari hadi kwenye ofisi za Manispaa ya Kinondoni na kuzungumza na Mganga Mkuu wa Manispaa, Festo John ambaye alisema ni kweli watu waliokumbwa na kadhia hiyo wapo na si jambo la siri lakini yeye si msemaji.
“Watumishi waliokumbwa na kadhia hiyo wapo kweli na si jambo la siri lakini mwenye mamlaka ya kutoa taarifa hizo zaidi ni mkurungezi kwa sababu yeye ndiye msemaji,” alisema John.
Gazeti hili lilikwenda kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni lakini halikuweza kufanikiwa kuonana naye maana alikuwa na majukumu ya kikazi badala yake likafanikiwa kuzungumza na afisa uhusiano ambaye pia alisema hayupo kwenye nafasi ya kulizungumzia hilo. Akasema mkurugenzi wa manispaa ndiye hasa anayeweza kuzungumza zaidi.
Rais Magufuli aliwataka wafanyakazi wote wa umma wenye vyeti feki kujiengua wenyewe kabla ya Mei 15, mwaka huu. Huku kwa wale ambao watakaidi basi watafikishwa mahakamani kwa kesi ya kughushi.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu alipopigiwa simu, iliita bila kupokelewa.