Sweetbert Lukonge|CHAMPIONI| Dar es Salaam
SIMBA jana waliunguruma tena na kurejea tena kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa African Lyon kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Ibrahim Ajibu alihusika kufunga bao moja lakini bao la kujifunga la Lyon lilizima kelele zote za Yanga Uwanja wa Taifa, kwani mashabiki wa wapinzani hao walikuwa wakipiga kelele nyingi baada ya Lyon kusawazisha. Sasa Simba ipo fainali ya Kombe la FA na ina uwezekano pia wa kutwaa ubingwa wa Bara.
Simba wamepata ushindi huu siku moja baada ya Yanga kuwachapa Prisons mabao 2-0 na kukaa kileleni mwa Ligi Kuu Bara kwa saa 24 wakiwa na pointi 59, ambapo sasa Simba wamekaa kileleni na pointi 62, ingawa Simba wamebakiza michezo miwili na Yanga minne.
Hii ni sawa na Simba kulipa kisasi kwa kuwa kwenye mchezo wa kwanza wa ligi kuu uliopigwa kwenye uwanja huo, Simba walilala kwa bao 1-0 dhidi ya Lyon.
Hata hivyo, hii ni mara ya tatu Simba na Lyon wanakutana msimu huu kwa kuwa walikutana tena kwenye mchezo wa hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA ambapo Simba walishinda bao 1-0.
Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu alikuwa wa kwanza kufunga bao kwenye mchezo huo kwa shuti la mbali katika dakika ya 37.
Kabla mpira huo haujaingia wavuni ulimgusa beki wa zamani wa Simba, Rajab Isihaka na kumpoteza kipa wa Lyon.
Hili lilikuwa bao la saba kwa Ajibu msimu huu wa ligi na kuonyesha kuwa anaweza kumaliza vizuri msimu huu.
Wakati zikiongezwa dakika nne kabla ya mapumziko, Simba walifanya kosa na kumuachia Omary Abdallah ambaye alipiga shuti kali kutoka nje ya eneo la 18 ambalo lilitinga wavuni moja kwa moja na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuonyesha kiwango cha hali ya juu na kucheza soka safi ambapo juhudi zao zilizaa matunda katika dakika ya 55 ambapo Hamad Waziri alijifunga wakati akijaribu kuokoa hatari langoni mwake.
Katika dakika ya 74, Ajibu alipiga shuti kali kutoka nje ya 18 ambapo ulimshinda kipa wa Lyon lakini ukagonga mwamba na kurudi uwanjani.
Simba walionekana kucheza kwa utulivu mkubwa sana kipindi cha pili, lakini wakiwa na umakini wa hali ya juu kutokana na hofu kubwa kuwa Lyon wanaweza kurudisha.
“Tunamshukuru Mungu kwa matokeo tuliyopata, tumebakiza michezo miwili na tunaweza kubaki kwenye ligi,” alisema Hamadi Wazir.
Makipa wa timu zote mbili hawakuwa na raha langoni mwao kutokana na katikati ya magoli yote mawili kujaa tope.
Huu ulikuwa mchezo mwingine ambao Simba walikuwa wanacheza dhidi ya wachezaji wengi ambao waliwahi kucheza kwenye timu hiyo.
Wachezaji wanne ambao ni Miraj Adam, Peter Mwaliyanzi, Rajab Isihaka na Omary Waziri ni kati ya wachezaji ambao walianza kwenye mchezo huo wakiwa waliwahi kuichezea Simba.
Hata hivyo, mechi ya jana ilikuwa na mashabiki wachache sana kuliko
michezo mingine kadhaa iliyopita ambayo imewahusisha Simba msimu huu.
“Matokeo haya ni faraja kwetu, African Lyon walikuwa wa kwanza kutufunga mchezo wa mzunguko wa kwanza, naamini kuwa tutacheza vizuri michezo yetu miwili iliyobaki,” alisema nahodha wa Simba, Jonas Mkude.