WAKATI serikali inatambua mchango mkubwa wa wanawake katika shughuli za maendeleo, imewataka pia wanaume kuwaunga mkono wanawake katika kuchangia maendeleo ya taifa kwa jumla.
Wito huo umetolewa jana na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, wakati wa uzinduzi wa vikundi vya akina mama vya Wanawake Live uliofanyika Pugu kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Meya Mwita alisema kina mama ndiyo msingi mkubwa ndani ya familia na taifa kutokana na mchango ambao wanautoa, jambo ambalo linaloleta ustawi mkubwa kimaendeleo.
Aliongeza kuwa licha ya changamoto ambazo hukutana nazo lakini wamekuwa ni watu wasiokata tama, hivyo akasisitiza kuwa kinababa wanatakiwa kutoa ushirikiano wao pia.
Aidha aliwapongeza wa kinamama kutokana na ubunifu wanaokuwa nao kila kukicha katika kujitafutia maendeleo na hivyo kuwa msaada mkubwa ndani ya familia zao ikiwemo kuwasaidia majukumu kinababa.
“Natambua mchango wenu sana, mmekuwa wabunifu , mnajishughulisha kwenye mambo mbalimbali ya kimaendeleo, mmekuwa mstari wa mbele kutengeneza miradi ambayo inasaidia kwenye familia zenu bila hata kinababa kushiriki.