


NA GLADNESS MALLYA | RISASI JUMAMOSI | MPAKA HOME
KILA Jumamosi huwa tunakutana katika safu hii ya Mpaka Home mpenzi msomaji ambapo tunatembelea nyumba za wasanii mbalimbali na kuona vitu wanavyovifanya wakiwa majumbani mwao tofauti na kazi zao za sanaa.

Leo tumemtembelea msanii wa filamu za Kibongo, Mwanaheri Ahmed anayeishi maeneo ya Kijitonyama, Dar na ameeleza mambo ambayo hupenda kuyafanya akiwa nyumbani.

MPAKA HOME: Nyumbani kwako pametulia sana, vipi unaishi na nani?
MWANAHERI: Naishi na dada yangu.
MPAKA HOME: Hebu tuambie ratiba yako kwa siku inakuwaje?

MWANAHERI: Nikiamka asubuhi chakwanza huwa naamkia bafuni kuoga si unajua tena mwanamke usafi, baada ya hapo ndiyo huwa naanza kazi za usafi wa mazingira na ndani ya nyumba yangu.
MPAKA HOME: Naona kama kuna biashara unafanya hapa nyumbani, ni biashara gani?
MWANAHERI: Nafanya biashara ya Madera na urembo mbalimbali wa wanawake na huwa nafanyia hapahapa nyumbani kwa kutumia simu yangu ya mkononi, wateja wengine wakihitaji nawapelekea walipo.

MPAKA HOME: Huwa unapenda kuvaa mavazi ya aina gani uwapo nyumbani?
MWANAHERI: Inategemea nafanya nini maana kila kazi na vazi lake, mara nyingi nikiwa nafanya usafi huwa napenda kuvaa taiti na blauzi ndefu ili kuwa huru zaidi, nikiwa napika navaa dera, nikiwa naangalia muvi huwa napenda kuvaa nguo nzuri za kuvutia kwani muda huo huwa nakaa sebuleni ni rahisi wageni kunikuta hapo, kutokana na hadhi yangu huwa napenda kupendeza.
MPAKA HOME: Ni chakula gani unachopenda kukipika?

MWANAHERI: Napenda sana kuchoma nyama maana huwa sipendi kula za barabarani, chakula kingine ni wali wa nazi na rosti ya nyama ya kuku.
MPAKA HOME: Tunashukuru kwa ushirikiano wako.
MWANAHERI: Ahsante na karibuni tena wakati mwingine.
