×

Wizi Mpya Helmet za Bodaboda Jijini Dar

STORI NA MWANDISHI WETU | IJUMAA | HABARI

WAKATI Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Usalama Barabarani likisisitiza abiria na madereva wa bodaboda kuvaa kofia ngumu ‘helmet’, baadhi ya madereva wezi wa kifaa hicho cha moto wamebuni mbinu mpya ya kuwaibia abiria kwa kutumia kofia hizo. Kitengo Maalum cha Oparesheni Fichua Maovu cha Global Publishers (OFM) katika siku za hivi karibuni kilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu wakieleza jinsi ndugu zao walivyofanyiwa kitu mbaya baada ya kupanda bodaboda za watu hao wahalifu.

MSIKIE HUYU

Mmoja wa wasomaji wetu aliyejitambulisha kwa jina la Sakina Malei wa Mbezi Mwisho jijini Dar aliliambia Ijumaa kuwa, hivi karibuni ndugu yake alipanda bodaboda katika maeneo ya Mbezi Kwa Msuguri lakini baada ya hapo hakujua kilichotokea hadi alipojikuta yupo kichakani na kila kitu kimekwenda.

“Mimi yule ndugu yangu alifikwa na mkasa mzito, alichukua bodaboda, alipopanda akapewa helmet avae, kumbe sasa kwenye ile helmet sehemu ya mdomoni kuna vitu wanaweka, sijui ni madawa au nini, wakafika eneo f’lani lina kichaka, akawa amepoteza fahamu na ndipo walipomuibia kila kitu,” alisimulia dada huyo.

Siku nyingine pia alipiga simu kijana mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini na kusema: “Jamani kuna mbinu mpya ya wizi ambayo baadhi ya wahalifu wanaitumia, hii ni ya kuvalishwa helmet zenye dawa za kulenya, ukishazima wanakuibia kila kitu.

Hili liwe fundisho kwa watu kutojipandia bodaboda ovyo. “Wengi wamelizwa kwa mbinu hii na kibaya zaidi wanawaharibia wenzao wanaofanya biashara ya bodaboda. Hivi kweli ndiyo iwe kila anayepanda bodaboda awe na kofia yake, itawezekana
kweli?” alihoji kijana huyo.

NI MAENEO MENGI JIJINI DAR

Kufuatia malalamiko hayo, OFM iliamua kufanya ‘ufukunyuku’ wake kwa kuzungumza na watu wengine na kubaini kuwa wizi huo umekuwa ukifanyika hasa maeneo ya Mbagala, Kilungule, Tabata na sehemu za pembezoni mwa Jiji la Dar.

WASIKIE MADEREVA BODABODA

Baadhi ya madereva kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar waliliambia gazeti hili kwamba, pamoja na ukweli wa uwepo kwa matukio ya namna hiyo, lakini mara nyingi matendo hayo yanafanywa na waendesha bodaboda wanaopaki katika vituo ambavyo havijasajiliwa.

“Wizi wa namna hiyo nishausikia sana tu, kwa upande wangu hapa kijiweni kwetu hakuna kitu cha namna hiyo, mara nyingi wizi wa hivyo unafanywa na madereva wanaopaki kwenye vijiwe ambavyo havina usajili wa kisheria,” alisema Nasri Ismali, muendesha bodaboda wa Kinondoni.

Naye Thabit Foize wa Ilala alisema,  wizi wa namna hiyo upo na umeshika kasi zaidi sehemu ambazo zipo pembeni ya mji na hufanywa hasa nyakati za usiku na baadhi ya madereva wenye tamaa ya pesa na mali.

Kufuatia uhalifu huo, waandishi wetu walifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Suzana Kaganda lakini hakupatikana ila kaimu wake, Juma Bwire alisema hawana taarifa ya aina hiyo ya uhalifu ila kwa kuwa taarifa zimewafikia, watazifanyia kazi. Kamanda wa Temeke, Gilles Muroto na wa Ilala, Salum Hamdani hawakuweza kupatikana mara moja.

Hata hivyo, gazeti hili linawatahadharisha wananchi wanaotumia usafiri wa bodaboda kuchukua tahadhari juu ya wizi huu mpya na kwa kuwa kutovaa helmet nako ni kosa kisheria, si vibaya kama ni mtumiaji wa usafiri huo mara kwa mara ukawa na kofia yako.

Leave a Comment