
Ibrahim Mussa| CHAMPIONI | Dar es salaam
NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, amefunguka kuwa sababu ya kushindwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Lesotho ni kutokana na udogo wa uwanja, hali iliyowafanya washindwe kufunguka.
Juzi Jumamosi usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar, Taifa Stars ilipambana na Lesotho ukiwa ni mchezo wa Kundi L ambao ulimalizika kwa matokeo ya sare ya 1-1 huku Samatta
akifunga bao hilo moja.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Samatta alisema kuwa wamechukizwa na matokeo hayo ya sare waliyoyapata kwa kuwa hayakuwa matarajio yao kutokana na ubora waliokuwa nao.
“Ukiangalia Uwanja wa Taifa na huu (Azam Complex) ni tofauti, kule Taifa ukicheza unakuwa na uhuru na nafasi zinaonekana lakini hapa kitu kilichowasaidia Lesotho ni kutokana na uwanja kuwa mdogo kwa sababu waliweza kuzuia nafasi zote, mipira yote iliyokuja nyuma waliweza kuicheza kwa urahisi kwani kila eneo mchezaji wao alikuwepo.
“Uwanja umewasaidia lakini vilevile suala la kuonekana kama nina hasira, kawaida mimi huwa sipendi kushindwa, matokeo ya sare sijayafurahia, tulikuwa tunacheza nyumbani na ukiangalia ni hatua ya makundi, tulikuwa tunahitaji ushindi katika hali yoyote ili tujiweke katika mazingira mazuri na siyo peke yangu niliyechukizwa na matokeo haya, karibu wachezaji wote,” alisema Samatta.