
SAID Mohamed ‘Nduda’ ni kipa wa Simba ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro a m b a p o hadi sasa hajaichezea mechi hata moja katika Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2017/18, sababu kubwa ni kutokana na kuwa majeruhi.
Nduda ambaye ndiye kipa bora wa michuano ya Cosafa iliyofanyika nchini Afrika Kusini hivi karibuni, alianza kuugua goti tangu alipokuwa katika maandalizi ya msimu huu wakati timu yake ikijiandaa kucheza dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii wakati huo Simba ilikuwa visiwani Zanzibar.
Tangu hapo amekuwa nje ya uwanja hadi hivi sasa huku ikielezwa kuwa anajiandaa kwa safari ya kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi.
Safari yake hiyo imekuwa ikipigwa danadana kila kukicha. Gazeti la Championi Ijumaa limekutana na kipa huyo wa zamani wa Yanga, na hapa anafunguka.
UNAZUNGUMZIAJE MAJERAHA YAKO?
“Nimekuwa katika wakati mgumu wa kuona goti lilianza muda mrefu tangu nilipokuwa na timu ya Mtibwa Sugar msimu uliopita ambapo lilikuwa likinisumbua japokuwa nilipatiwa matibabu.
“Baada ya matibabu niliendelea kuwa fiti na kufanya kazi zangu kama kawaida na hata katika mashindano ya Cosafa yaliyofanyika nchini Afrika Kusini hivi karibuni nilipokuwa timu ya taifa, tatizo hili halikujitokeza.
“Goti lilianza kunisumbua tena wakati najiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga iliyochezwa Agosti 23, imekua hivyo hadi sasa.
VIPI KUHUSU SAFARI YA INDIA?
“Upande wangu nausubiri uongozi ambao ndiyo umepanga safari hiyo na pindi itakapokamilika m i m i n i takuwa t a y a r i k w e n d a , awali kitu kilichokuwa kikikwamisha ilikuwa ‘visa’ lakini kwa sasa tayari nimeshaipata ila sijajua nini kinaendelea na mimi nawasikiliza wao ndiyo wenye maamuzi ya mwisho.
KWA SASA UNAFANYA SHUGHULI GANI?
“Natumia muda mwingi kujipumzisha ili kujiweka sawa kimwili na kiakili kwa sababu hivi sasa naendelea na matibabu tu ya hapahapa huku nikisubiri safari. Sina shughuli nyingine yoyote ninayoifanya nje ya mpira zaidi ya kusikilizia afya yangu.
UNAZUNGUMZIAJE KUKAA NJE MUDA MREFU?
“Ni kweli niliambiwa kuwa pindi nitakaporejea nitakaa nje ndani ya wiki nne hadi sita bila ya kufanya shughuli yoyote ya kimpira, kwa upande wangu sijisikii vizuri, lakini naamini nitakapopata nafuu nitarudi katika hali yangu.
UNADHANI MAJERUHI YATAKUPOTEZEA NAMBA?
“Ushindani wa namba ndani ya Simba upo mkubwa sana na hasa ukizingatia kila mchezaji anahitaji kucheza, kikosi chetu ni kipana kwa sasa, lakini mwisho wa siku mwalimu ndiyo mtu wa mwisho kufanya maamuzi ampange nani.
“Kwa upande wangu sina tatizo lolote juu ya uwepo wa (Aishi) Manula ila najua nikipona nitapata nafasi ya kucheza, kikubwa zaidi ni kujituma katika mazoezi ili kuendelea kuwa fiti kwani ninauamini uwezo wangu.
NENO LAKO KWA SIMBA KATIKA MBIO ZA UBINGWA MSIMU HUU?
“Kuzungumzia suala la ubingwa kwa sasa ni mapema mno japokuwa moja ya malengo yetu ni kuona tunafanikiwa kuwa mabingwa msimu huu, hasa ukizingatia usajili uliofanywa msimu huu ni mzuri.
“Kitu cha msingi ni kuona tunafanikiwa kushinda katika kila mchezo ili iweze kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi, kila mchezaji angependa kuona tunafanikiwa mwisho wa msimu.
UNAZUNGUMZIAJE UWEPO WA OKWI, NIYONZIMA NDANI YA SIMBA?
“Wachezaji hawa ni maprofesheno hivyo uwepo wao kikosini kuna umuhimu wa hali ya juu na watatoa msaada mkubwa kuhakikisha wanaisaidia timu kufika kule ambapo imetarajia kufika.
“Mfano mzuri tunaweza kuona jinsi Okwi anavyoifungia timu kwa sasa ambapo hadi sasa ana mabao sita, hivyo ni mwanzo mzuri.”