
KATIKA kuhakikisha anapunguza tofauti ya idadi ya mabao waliyonayo dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina amewapa mbinu mbadala washambuliaji wake tegemeo Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni saa chache kabla ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida United utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida.
Simba hadi hivi sasa tayari imefanikiwa kufunga mabao 20 huku ikiruhusu mabao matano na Yanga ikifunga mabao 11 na kufungwa manne katika mechi nane walizocheza za ligi hiyo kwa msimu huu.

Kocha huyo alionekana akiwapa mbinu hizo kwenye mazoezi ya mwisho yaliyofanyika juzi Jumatano asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar kabla ya kuelekea Singida kuvaana na wapinzani wao hao.
Katika mazoezi hayo, Lwandamina alionekana akiwapa mbinu za kufunga washambuliaji wake hao kwa kufunga mipira ya krosi kwa njia ya kichwa na miguu kumchambua kipa.
Lwandamina aliwataka Ajibu na Chirwa kufunga mabao ya umbali tofauti ya mita 20 na 18 kwa kupiga mashuti na kumchambua kipa aliyekuwepo golini ambaye ni Beno Kakolanya.
Mzambia huyo aliwatumia mabeki wa pembeni Hassan Kessy, Gadiel Michael na viungo wa pembeni, Pius Busitwa na Geofrey Mwashiuya kwa ajili ya kupiga mipira ya krosi kwa washambuliaji hao.
Wakati mwingine kocha huyo, alionekana kutumia mbinu za kufunga wakitumia njia ya katikati kupenya safu ya ulinzi ya kati akimtumia Raphael Daudi, Kabamba Tshishimbi na Ajibu kumtengenezea pasi za mabao Chirwa.
Kocha huyo, alitumia programu hiyo ya mazoezi kwa saa mbili, yalianza saa 3:00 na kumalizika saa 5:00 asubuhi.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Singida, Lwandamina alisema: “Kikubwa tumejipanga vema kuhakikisha tunashinda mechi na Singida ili tujiweke katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kuu.
“Kitu kikubwa tunachotakiwa kukifanya ni kutumia vema kila nafasi tutakayoipata ya kufunga mabao ili tupate ushindi, kwani mechi iliyopita na Simba tulipoteza nafasi nyingi.”
Stori: Wilbert Molandi na Musa Mateja