
Hatimaye Jengo la Wizara ya Maji na Umwagiliaji lililo ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam limeanza kubomolewa leo Jumatatu, Novemba 27, kutekeleza agizo la Rais, Dkt. John Magufuli.
Rais Magufuli aliagiza majengo ya wizara hiyo na ghorofa la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwekwa alama ya X na kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo kwa kuwa yako ndani ya hifadhi ya barabara.
Akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Novemba 15,2017, Rais Magufuli akiwa na makamu wake, Bi Samia Suluhu aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.
Katika majengo ya Wizara ya Maji, tingatinga limevunja ukuta, huku watu wengine wakiendelea na kazi ya kuondoa madirisha na milango kwenye majengo. Jengo lililoanza kubomolewa ni la Ofisi ya Waziri wa Maji.

Wafanyakazi wa wizara hiyo wanaendelea kutoa mali ndani ya majengo waliyokuwa wakiyatumia kwa ofisi.
Mbali ya majengo hayo, Tanraods inaendelea kuweka alama ya X kwenye nyumba za wananchi zilizo katika hifadhi ya barabara ikiwa ni pamoja na kupisha ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo.
Tayari nyumba takriban 1,200 zikiwamo tano za ibada, vituo vya mafuta na baa katika eneo la Ubungo hadi Kimara Mwisho zimewekwa alama kwa ajili ya ubomoaji.
Kwa mujibu wa Tanroads, ubomoaji katika eneo la Ubungo hadi Kimara Mwisho unahusisha nyumba zilizo mita 91.7 katika hifadhi ya barabara ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Barabara ya mwaka 1932.
Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers
Android ===>Google Play
iOS ===>Apple Store
VIDEO YA TUKIO HILO