
UONGOZI wa Klabu ya Simba kupitia kwa kamati yake ya usajili inayoongozwa na mwenyekiti wake, Zakaria Hans Poppe, umelitolea ufafanua sakata la usajili wa beki wa kati, Asante Kwasi.
Kwasi ambaye mwanzoni mwa msimu huu aliichezea Lipuli FC ya Iringa, inaelezwa ameshasajiliwa na Simba lakini kuna mvutano juu ya usajili wake ambapo Hans Poppe amezungumza na kwa kauli zake inaonyesha wazi Kwasi ataichezea Simba.
Habari ni kuwa licha ya sakata hilo kuendelea lakini Simba ambayo itashuka uwanjani leo Ijumaa kucheza dhidi ya Green Warriors katika Kombe la FA, imepanga kumtumia mchezaji huyo ikiwa kila kitu kitaenda sawa.

Kamati hiyo iliiandikia barua Lipuli juu ya kumhitaji mchezaji huyo raia wa Ghana ikiwa ni muda mfupi baada ya wao kumalizana na wakala wa Kwasi, Godwin Emmanuel ambaye alikuja nchini kumalizana kila kitu na vigogo hao wa Msimbazi.
Akizungumzia sakata hilo, Hans Poppe amenukuliwa akisema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kupata ridhaa ya Lipuli baada ya kumalizana na wakala wa Kwasi ambaye ndiye mwenye ridhaa ya kummiliki nyota huyo ambapo kwa sasa wanasubiria majibu kutoka kwa Wanapaluhengo hao.
“Ni kweli Simba tunamtaka Kwasi aje achezee timu yetu na tumewaandika barua rasmi Lipuli ya kumtaka mchezaji huyo, tunaamini kwenye siku hizi mbili tatu za dirisha dogo lililosogezwa mbele (hadi Desemba 23) kila kitu kitakuwa vizuri.
“Unajua kabla ya kufuatilia mchezaji ni lazima ufuatilie mikataba yake na sisi tumefuatilia na kukuta kwamba hakuna timu ambayo inammiliki, hata hao Lipuli hawammiliki, ndiyo maana tukaongea na wakala wake na kumalizana naye.
“Niwahakikishie tu Wanasimba kama Kwasi atatua klabuni kwetu basi atakuja bila ya kufanya ubabe wowote ule yaani atakuja huru, hakuna sababu ya sisi kufanya ubabe kwa wenzetu, sisi tulikuwa tunaangalia namna ya kumnasa bila ya matatizo yoyote yale lakini wenzetu wakaona kwamba tunafanya njia zisizofaa,” alisema Hans Poppe.
LIPULI WAPOKEA BARUA
Mwenyekiti wa Lipuli, Ramadhan Maono amekiri kupokea barua hiyo lakini akadai kuwa wameweka ngumu kwa kusema ili wamuachie beki huyo raia wa Ghana kuna kiwango cha fedha ambacho wanakihitaji.
SIMBA KUMTAMBULISHA KWASI LEO
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilikutana jana kujadili mambo kadhaa likiwemo suala hilo ambapo inaelezwa Simba wametuma maombi maalum ili mchezaji huyo aruhusiwe kucheza katika mchezo wao wa leo wa FA Cup utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.
“Kwasi tumeshamalizana naye kila kitu, tumetuma maombi ya kumtumia Kwasi katika mchezo wa kesho (leo), kikao cha kamati ya TFF kimeahirisha suala hilo hadi kesho (leo), tulikubali kutoa shilingi milioni 50 ili tumalizane nao lakini wao Lipuli wameweka ngumu, sijajua wanataka kiasi gani lakini wamekataa dau tunalotaka kuwapa.
“Unajua kuna vitu vinaendelea kwao ndiyo maana unaona kuna taarifa baadhi ya viongozi wao wanachunguzwa kuhusu masuala ya fedha, lakini kikao kitakachokaa kesho (leo) asubuhi kitapitisha kama tunaweza kumtumia Kwasi katika mchezo huo au la,” alisema mtoa taarifa kutoka Simba.