WAKATI Simba wakiota ndoto ya mwisho pale Mtwara usiku wa kuamkia leo Ijumaa, huku Dar es Salaam bosi wao aliyepigwa chini, Joseph Omog alikuwa akipakia mabegi yake saba kwenye mwewe tayari kwa safari ya kurudi kwao Cameroon.
Wala alikuwa hajanuna au kukunja sura kwasababu alikuwa na ofa zake tano mkononi kutoka timu mbalimbali huku ikitajwa kwamba ana uwezekano mkubwa wa kuibukia Sudan.
Omog ambaye Jumamosi iliyopita alisitishiwa mkataba wake Msimbazi kutokana na kile kilichoelezwa ni matokeo mabovu ya timu hiyo, aliondoka usiku wa saa 9:45 kwa ndege ya Shirika la Kenya ‘KQ’.
Championi Jumamosi ambalo lilikuwepo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, lilimshuhudia Omog akiwasili uwanjani hapo saa 7:50 usiku tayari kwa safari yake.
Omog alionekana akiwa na mabegi saba yaliyoonekana kushiba vitu ndani yake kwani ndiyo anarudi moja kwa moja kwao mpaka atakapozipitia upya ofa alizonazo.
Akizungumza na Championi Jumamosi uwanjani hapo, Omog alisema anaondoka kwenda kwao kupumzika kwa mwezi mmoja, kisha ndiyo ataangalia mustakabali wa wapi aende kufanya kazi.
“Nimemalizana na Simba kwa kila kitu ndiyo maana naondoka, siwezi kuzungumzia zaidi timu ya hapo kwa kuwa sipo tena ndani ya timu hiyo ila nawatakia kila la heri,” alisema Omog.
Kwa sasa nafasi ya Simba inashikiliwa kwa muda na Kocha Msaidizi Masoud Djuma raia wa Burundi. Omog alitimuliwa baada ya Simba kuvuliwa ubingwa wa Kombe la FA na Green Warriors ya Mwenge jijini Dar es Salaam kwa penalti 4-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Omary Mdose, Dar es Salaam