
Musa Mateja | CHAMPIONI| Dar es Salaam
HAKIKA kipigo cha Simba kwa watani wao Yanga, kimemvuruga waziwazi kiungo wa Yanga raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima baada ya kutamka wazi kuwa muda mwingi amekuwa akiwaza ni kwa namna gani walipoteza. Niyonzima amejikuta kwenye hali hiyo baada ya timu yake kufungwa na Simba mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatano, Niyonzima ambaye kwenye mchezo huo alikuwa nahodha, alisema tangu kumalizika kwa mchezo huo, amekuwa na mawazo mengi sana juu ya timu yake kama itakuwa na uwezo wa kutetea ubingwa wao wa ligi.
“Tangu siku ile nimekuwa nikiwaza ni kwa namna gani tunaweza kushinda mechi zetu zilizosalia ili tuweze kutetea ubingwa wetu wa ligi tuliouchukua msimu uliopita. “Najua uwezo wa kupambana tunao, kuhakikisha tunatimiza malengo yetu, lakini kama hatutakuwa pamoja, hatuwezi kufanikisha hilo, hicho ndicho kinanifanya niwaze sana.
“Kama hakutakuwa na hujuma zozote zile dhidi yetu hakika tutashinda kila mchezo hadi mwisho kwa sababu kila mmoja aliyecheza siku ile aliumia na hakuna atakayekuwa tayari kuona tunafungwa tena,” alisema Niyonzima.
Ligi Kuu Bara imebakiza wastani wa michezo saba kwa kila timu, Simba wakiwa kileleni kwa sasa wakiwa pointi tano mbele lakini wakiwa wamecheza mchezo mmoja zaidi ya Yanga.