×

Yanga SC: Mwadui Kaeni Mbali Kabisa

BENCHI la ufundi la Yanga chini ya kocha wake mkuu, George Lwandamina limeibuka na kuwapiga biti wapinzani wao Mwadui FC kwa kuwaambia kuwa wamewaandalia kipigo ikiwa ni njia mojawapo ya kutuliza hasira zao tangu walipotolewa katika Kombe la Mapinduzi.

Yanga keshokutwa Jumatano watakuwa wenyeji wa Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa jijini Dar katika muendelezo wa ligi kuu, ambapo kwa sasa wanakamata nafasi ya tano wakiwa na pointi 21.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Lwandamina amesema kuwa wanataka kushinda mchezo huo kwa ajili ya kutuliza hali ya presha ambayo ipo kwa mashabiki wao lakini pia kujirudisha katika mbio za ubingwa.

“Tunataka kushinda mechi na Mwadui FC kwa ajili ya kurejesha hali sawa ndani yetu, kwani kama unavyokumbuka mara ya mwisho kwenye ligi tuliweza kupoteza mechi na Mbao FC lakini pia katika Kombe la Mapinduzi hatukufanya vizuri sana baada ya kutolewa nusu fainali.

 

“Mambo hayo yanafanya tuingie uwanjani kwa nia kubwa ya kutaka kushinda, tunaamini tukipata ushindi katika mchezo huu kila kitu kitakuwa sawa na pia tutarejea kwenye mbio za kutetea tena ubingwa wetu,” alisema kocha huyo raia wa Zambia.

Said Ally, Dar es Salaam