KIFO cha ghafla cha mwanamitindo au Video Queen wa Bongo Fleva, Agness Gerald almaarufu Masogange, kimeibua mshtuko mkubwa.
Jana, jioni, gazeti hili lilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Masogange kilichotokea kwenye Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge jijini Dar.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Afisa Habari wa Chama cha Waigizaji wa Wilaya ya Kinondoni, Dar, Masoud Kaftany aliliambia gazeti hili kuwa, kifo hicho kilijiri majira ya saa 10:30 jioni ambapo mwili wake ulipelekwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
“Ni kweli na mimi nimepata taarifa hizo na amepelekwa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi,” alithibitisha Kaftany.
Taarifa za awali zilizopatikana hospitalini hapo mara tu baada ya kifo hicho zilieleza kwamba, Masogange alikuwa akisumbuliwa na Ugonjwa wa Homa ya Tumbo (Typhoid Fever) na Upungufu wa Damu Mwilini (Anaemia).
MASOGANGE NI NANI?
Kabla ya kukutwa na umauti, mtu alipokuwa akizungumzia warembo wazuri ndani ya Jiji la Dar ni wazi kwamba asingeacha kulitaja jina la Masogange.
Jina la Masogange lilikuwa kubwa mno kutokana na kujishughulisha na upambaji wa video za wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva.
Kumbukumbu kwenye makabrasha ya gazeti hili zinaonesha kuwa, Masogange alizaliwa Aprili 23, 1988 kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mbeya. Masogange alisoma katika shule ya Msingi na Sekondari ya Sangu jijini Mbeya kabla ya kuendelea na kidato cha tano na sita na baadaye alitinga jijini Dar katika harakati za kutafuta maisha.
Aliingia katika kazi ya uanamitindo kupitia video za wanamuziki mbalimbali kutokana na umbo lake matata lilionekana kuwa na mvuto kwenye video hizo.
Masogange ametokea katika familia ya wacha Mungu na kwamba wazazi wake hawakuafikiana naye katika kujishughulisha na kazi ya kuuza sura katika video za wasanii wa muziki wa kidunia.
Katika mahojiano mbalimbali na Magazeti ya Global, Masogange alieleza kuwa ana shughuli zake binafsi ambazo zilikuwa zikimuingizia fedha kumudu kuendesha maisha yake. Wengi hawajui, lakini Masogange ameacha mtoto mmoja wa kike.
Masogange alianza kuvuma zaidi baada ya kuonekana kwenye video ya Wimbo wa Masogange wa msanii kutoka Morogoro, Abednego Damian almaarufu Belle 9 kisha alitumbulia kwenye Bongo Movies.
Jina lake lilizidi kuwa maarufu pale alipohusishwa na skendo ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine ambapo alikamatwa nchini Afrika Kusini na baadaye mahakama nchini humo ilikanusha kuwa dawa hizo hazikuwa za kulevya bali za matumizi ya kimaabara kwa ajili ya tiba za kibinadamu.
Ukiacha msala huo wa Afrika Kusini, mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimtaja kwenye orodha ya mastaa wanaotumia madawa ya kulevya hivyo kushikiliwa na kesi yake kuunguruma katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu, Dar.
Katika kesi hiyo, Aprili 3, mwaka huu, Masogange alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi milioni 1.5 kwa kosa la kutumia kutumia madawa ya kulevya aina ya Heroin na Oxazepam ambapo alikubali kulipa faini hiyo hivyo aliachiwa huru. Tangu hapo, Masogange hakuonekana tena hadi kuibuka kwa mshtuko wa kifo chake.
Global Group tunaungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Masogange katika kipindi hiki kigumu. Rest In Peace Masogange!
Mbali na Video ya Wimbo wa Masogange, video nyingine alizoonekana Masogange ni Magubegube ya msanii Barnaba Elias au Barnaba Boy na ile ya msanii Tundaman iitwayo Msambinungwa.
Comments are closed.