KWENU mastaa wa fani mbalimbali hapa nchini. Nawasalimu wote, kama unajijua wewe ni msanii wa fani yoyote, soma barua yangu ya leo na uifanyie kazi.
Kwa wiki ya pili sasa nazungumza nanyi kwa ujumla wenu kwani naona kuna kila sababu ya kufanya hivi, kuwaeleza kwamba nilichokisikia wiki iliyopita kutoka kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harison George Mwakyembe ni aibu!
Nilisikitika sana kusikia waziri anazungumzia suala la mchekeshaji mkongwe, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ kwamba kama waziri, ameombwa achangie kiasi cha shilingi laki tano kwa ajili ya matibabu ya staa huyo.
Ndugu zangu, sina maana ya kumzungumzia vibaya Majuto (najua anajimudu, pengine pia kuna mikataba alionewa) wala familia yake, lakini nalitazama suala hili kwa ujumla wake.
Tumeshuhudia mara kadhaa huko nyuma tukipitisha bakuli katika matatizo mbalimbali yanayowakumba wasanii.
Bahati mbaya sana, maisha yenu tunayajua, tunakutana kwenye vijiwe kila siku, mnateketeza fedha kama hamna akili nzuri bila kujua kesho yenu.
Kifupi mnajisahau. Mnaishi kanakwamba mnaitegemea leo tu, kesho hamna mpango nayo. Ni aibu yanapotokea haya halafu watu ambao wanaamini mpo vizuri wakasikia mnachangishana.
Kwa nini msijiwekee mfumo mzuri wa maisha yenu ambao utawafanya muweze kujimudu? Mnalalamika kwamba mnaibiwa, lakini mbona mnapata fedha ambazo mnazifuja na tunawaona kila siku?
Kwa nini msijilipie hata Bima za Afya na siku hizi zipo za aina nyingi? Ni aibu kwa msanii ambaye watu wamezoea kumuona kwenye luninga akionesha kwamba fedha kwake si tatizo halafu anapoumwa kidogo tu, tatizo!
Ndugu zangu, maisha ya sasa yamebadilika, kama tulikuwa tunaishi kiujanjaujanja, zile zama zimepita. Sasa hivi atakayefanya kazi tu ndiye atakayeweza kumudu gharama za maisha.
Niwaambie ukweli, hizi si zile zama za kukesha baa kila siku, mnapaswa kusoma alama za nyakati maana kama ni kupoteza muda, mlishapoteza sana hivyo ni wakati sasa wa kubadilika.
Ni wakati wa kila mmoja kujifanyia tathmini, ni wapi alikosea, nini afanye ili aweze kusimama upya na kubwa kuliko yote ni kujihakikishia kwamba unakuwa na ulinzi wa kesho yako.
Hakuna ajuaye kesho yake, lakini ni vyema kujiandalia kesho nzuri. Punguzeni starehe zisizo na maana. Simamieni kweli misingi ya haki katika kazi zenu. Kuweni na umoja, acheni unafiki na majungu.
Mnapoamua jambo lenu, asiwepo hata mmoja wa kwenda kinyume na wenzake. Tatizo lenu, wengi mmetawaliwa na unafiki. Mmetengeneza makundi ambayo yanawashinda kuyavunja miaka na miaka.
Badilikeni, hizi ni zama za kuoneshana umoja. Oneshaneni upendo, kama Mungu alivyotupenda sisi, basi na nanyi mpendane kwa dhati.
Siyo mdomoni mjifanye kusema mnapendana kumbe moyoni hakuna kitu. Hata michongo hamuwezi kupeana kama mnaishi kwa makundimakundi. Ndiyo maana mnabaniana, mtu yuko radhi amuunganishe msanii fulani katika dili fulani hata kama hana vigezo husika.
Wakati mwenye vigezo yupo, hampi kwa sababu tu hawaongei au yupo kundi la tofauti na yeye. Jamani huo ni ushamba wa hali ya juu, msiishi hivyo.
Pendaneni, saidianeni na mtainuka wote kama mastaa wa Bongo Movies, Bongo Fleva na tasnia nyingine.
Mungu awabariki, ninawatakia mabadiliko mema.
Mimi ni ndugu yenu;
Erick Evarist.