×

JPM Akagua Mafuta Yenye Utata Bandarini, Atoa Maagizo – VIDEO

RAIS John Magufuli leo Jumanne, Mei 15, 2018 amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam na kumaliza utata wa sakata la mafuta huku akiagiza kampuni tatu kulipa asilimia 25 ya kodi baada ya kubaini matanki saba kati ya yaliyokaguliwa na TBS yana mafuta safi yanayofaa kwa ajili ya matumizi.

 

“Baada ya uchunguzi kufanyika imebainika kwenye matanki hayo yapo ambayo yalikuwa na ‘crude oil’, na mengine yalikuwa na ‘refined oil’ ambayo yalifichwa,” alisema Rais Magufuli.

Pia, ameagiza kampuni hizo zitozwe faini kwa kudanganya kuwa ziliingiza bandarini mafuta ghafi wakati zikitambua kuwa ni masafi na yanafaa kutumika.

 

“Katika mafuta waliyosema ni crude kumbe ni refined walipe asilimia 25 pamoja na faini, yale ambayo ni crude walipe asilimia 10 kwa mujibu wa sheria za TRA, hayo ambayo ni safi utaratibu unyanyike walipie haraka yatoke hapa yapelekwe sokoni, hatuwezi tukawa tunaibiwa kila siku tunahitaji kujenga viwanda vyetu,” alisema Rais Magufuli.

 

Aidha, ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa kuchukua sampuli katika matanki yenye mafuta hayo, mamlaka hizo zilibaini kuwapo kwa matanki yenye mafuta safi (refined oil), mafuta ghafi (crude oil) na malighafi ya kutengenezea sabuni.

 

Mbali na hayo, Rais amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage,  kupeleka muswada bungeni kwa ajili ya kubadili sheria ya kodi ili wanaoingiza mafuta nchini watozwe kodi kubwa kulinda ukuaji wa viwanda vya ndani kwa maslahi ya taifa.

 

“Hii sheria yetu inawezekana kulifanyika kamchezo, wabunge wajadili na kupitisha kitu kingine, kilicholetwa huku kusainiwa ni kingine, haiwezekani crude oil ukachaji sawa na semi refined,” alisema Rais Magufuli.

RAIS MAGUFULI AKIZUNGUMZA BAADA YA ZIARA HIYO