×

Watanzania 11 Walioshitakiwa kwa Ubakaji Waachiwa Afrika Kusini

VIJANA 11 raia wa Tanzania waishio Johannesburg, Afrika Kusini,  walioshtakiwa kosa la ubakaji wameachiliwa huru na hakimu mkazi wa Mahakama ya Johannesburg.

 

Watanzania hao walikuwa wameshtakiwa kwa makosa ya kumteka nyara na kumbaka mwanamke mjamzito aitwaye Thelma Mondowa, raia wa Zimbabwe mwaka uliopita.  Watuhumiwa hao waliachiliwa na Jaji Metisie kwa kukosekana ushahidi.

 

Wakili wa upande wa mashtaka wa serikali alikuwa amemfahamisha hakimu kuwa  Mondowa aliamua kurejea Zimbabwe hivyo upande wa mashtaka umeshindwa kupata anwani yake ya kuwasiliana naye.

 

Ilidaiwa mwanamke huyo alikuwa akitoka kazini na mfanyakazi mwenzake wa kiume ambapo walivamiwa na kundi la wanaume wenye silaha na wakamvuta mwanamke huyo kabla ya kumpiga mfanyakazi mwenzake ambaye alifanikiwa kutoroka.

 

Kisa hicho kinadaiwa kutokea Mei 15, 2015,  katika Barabara ya 270 Lilian Ngoyi mjini Johannesburg.

Baada ya mfanyakazi huyo kutoroka aliwapigia simu polisi na wakafanikiwa kufika eneo la tukio na kuwakuta wanaume hao wakimbaka kwa zamu mwanamke huyo.

Polisi wapatao kumi waliingia kwenye jengo ambapo tukio lilidaiwa kufanyika na kumuokoa mwanamke huyo na kumpeleka hospitalini.