
SIKU 14 zijazo dirisha rasmi la usajili wa Ligi Kuu Bara litafunguliwa, lakini vurugu kubwa zimeanza mitaani baada ya Simba, Yanga na Azam kuanza kujiweka mguu sawa.
Klabu hizo tayari zimeanza kufanya mazungumzo ya awali na kuwasainisha wachezaji wa timu pinzani waliomaliza mikataba, huku Yanga wakionekana wanyonge zaidi kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Kitendo cha Azam FC kumuajiri Kocha wa Singida United, Hans Pluijm kimeongeza vurugu zaidi kwenye usajili kwani Mholanzi huyo amepania kufanya kazi na mastaa wazoefu na ameanza kuvuna anakotoka pamoja na Yanga na Simba.

Beki kisiki wa Yanga, Juma Abdul atatangazwa rasmi na Azam Jumatatu ijayo, baada ya kuachana na Hassan Kessy ambaye anatokea pia Yanga na alikuwa kwenye orodha ya Pluijm ambaye hataki masihara msimu ujao.
Lakini Shiza Kichuya ambaye mkataba wake na Simba umefikia ukingoni, jana uvumi ulizagaa kwamba alinaswa na vigogo wa Yanga, lakini habari za ndani zinadai kuwa ana mchongo anausikilizia nje ya nchi.
Habari zinasema kwamba baba yake mzazi aitwaye Ramadhan Kichuya, anashinikiza aondoke Msimbazi lakini kama akibaki basi apewe mshahara mnono, huku mmoja wa watu wa karibu wa Mohammed Dewji akidai Kichuya ishu yake itamalizwa muda wowote na atabaki Simba.

Azam kiraka wao, Himid Mao, jana walimtangaza rasmi kwamba wanaachana naye na atakwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa ingawa machale yanawacheza kwamba huenda akapiga krosi kwenye taa za Kariakoo akaibukia Simba.
Yanga bado wameshika roho zao kwa beki wao, Kelvin Yondani ambaye licha ya kwamba jana walimuibukia kwake na kumleta klabuni kuzungumza naye lakini bado hawajiamini kwani Azam na Simba wanamtolea macho na akaunti zao zimetuna, ingawa ilielezwa hadi jioni walikuwa wanambembeleza asaini mkataba wa miaka miwili klabuni hapo.
Pluijm amefanya kazi na Yondani na anajua ubora wake huku Simba wakimtamani ili aboreshe ukuta wao na waachane na Juuko Murshid wa Uganda ambaye vigogo wengi wanaonekana kutomuamini.

Vurugu nyingine ya usajili ipo kwa Papy Kabamba Tshishimbi ambaye licha ya kuwa na mkataba na Yanga lakini vigogo wa Simba wamemuendea hewani na kumuahidi dau nono ambalo linashawishi kutumia wanasheria kukaa mezani kuvunja mkataba kikanuni.
Lakini juzi usiku, Yanga walikaa nae na kumuahidi mambo mazuri pamoja na kummalizia mzigo wake aliokuwa akidai akapanda ndege akaenda na kikosi hicho Nairobi kwenye mashindano ya SportPesa.
Ingawa straika Emmanuel Martin wa Yanga hatajwi sana lakini habari zinasema kwamba Singida United na moja ya timu zilizopanda daraja zinamuwinda na lolote linaweza kutokea ingawa Yanga wanaonekana kutokuwa na presha naye.
Yanga wanahusishwa na Juuko Murshid lakini bado Simba wanaamini kwamba wakimkutanisha na Mohamed Dewji ‘MO’ hachomoi.
Championi Ijumaa, linajua kwamba Simba wamefanya mazungumzo ya awali na straika wa Yanga, Obrey Chirwa lakini hawajafikia muafaka juu yake ingawa wengi wanashauri kwamba anafaa kuliko Laudit Mavugo ambaye alikuwa akipewa fungu kubwa la fedha lakini ufanisi hauonekani.
Viongozi wengi wa Simba wanaamini kwamba Chirwa alikuwa akizozana na Yanga kutokana na masilahi wala si mtovu wa nidhamu.
Beki Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Geofrey Mwashiuya wanatajwa kwenye listi ya Pluijm na inadaiwa kwamba kocha huyo amewaambia wasisaini mkataba mpya Jangwani kwanza lakini duru za ndani zinasema ana uwezekano mkubwa sana wa kumnyakua Dante kuliko Mwashiuya ambaye Azam ina wachezaji wengi wa aina yake.
Mohammed Ibrahim, ambaye alikorofishana na Kocha wa Simba, Pierre Lechantre hivi karibuni kutokana na utovu wa nidhamu, habari zinasema kwamba ameshasaini Yanga wiki mbili zilizopita huku Said Ndemla licha ya wakala wake kusisitiza anakwenda Denmark au Sweden, Simba machale yanawacheza kwamba anaweza kutambulishwa Yanga.
Lakini habari za moto ambazo Championi limezipata jana usiku ni kwamba Simba imeanza mazungumzo ya siri na straika Mtogo, Djako Arafat anayeichezea Woylaita Dicha ya Ethiopia ambaye Yanga wamemuweka mguu sawa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika amewasisitizia mashabiki wa klabu hiyo kwamba hawana papara na wanajipanga kufanya usajili mzuri wakianza na mastaa kumi ambao mikataba yao imemalizika.
