×

Yanga Fanyeni Haraka, Julai 18 Siyo Mbali

MABINGWA wa zamani wa Tanzania Bara, Yanga, ndiyo wamesalia kuwa wawakilishi wa Tanzania kwenye michua­no ya kimataifa kwa ngazi ya klabu.

 

Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika na sasa ipo hatua ya makundi. Tayari im­eshacheza mechi mbili na ku­jikusanyia pointi moja baada ya kupoteza mchezo wa kwan­za na ule wa pili ikitoka suluhu.

 

Hivi sasa wachezaji wa timu hiyo wapo kwenye mapumziko baada ya kumal­izika kwa msimu wa 2017/18, mapumziko hayo yamekuja muda mfupi timu hiyo ilipo­toka Kenya kwenye michuano ya SportPesa Super Cup iliyo­fanyika nchini humo kuanzia Juni 3 mpaka 10.

 

Inafahamika kwamba Yanga imejiondoa kwenye michuano ya Kombe Kagame iliyopangwa kuanza Juni 29, mwaka huu jijini Dar. Kujitoa kwao huko ni kwa sababu kuu mbili; moja wache­zaji walihitaji mapumziko zaidi kabla ya kucheza mechi yao ijayo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, la­kini pia ni kutokana na wache­zaji wao wengi wa kikosi cha kwanza kumaliza mikataba yao.

 

Baada ya hali hiyo, viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakifanya juhudi ya kuzun­gumza na nyota wao juu ya makubaliano ya mikataba mi­pya, lakini wakiwa kwenye mi­kakati hiyo, imeundwa kamati ya muda.

 

Ni muda mfupi kuanzia sasa mpaka mechi yao hiyo dhidi ya Gor Mahia, lakini bado hakuna jipya kwenye masuala yao ya usajili.

 

Maandalizi yao kwa ajili ya mchezo huo wamepanga kuanza Jumatatu ijayo, hivyo huu ni muda wa kamati yao hiyo ya usajili kufanya mambo haraka, isitokee zimebaki siku chache zaidi ndiyo wana­kuwa bize. Ikumbukeni Yanga inaburuza mkia kwenye kundi lao.

Bodi ya Uhariri/Maoni