
MTIBWA Sugar mnastahili pongezi kwa kuwa mmepambana mwanzo mwisho na hatimaye kuweza kubeba taji la ushindi katika mashindano ya kombe la Uhai ambalo lilihusisha timu za vijana.
Mechi zenu zote kwenu zilikuwa fainali hata mechi ya mwisho ilikuwa ni fainali na mkafanikiwa kuibuka na ushindi. Mnastahili pongezi maana lile bao mlilolipata linastahili kuwekwa kwenye kumbukumbu.
Sasa ni wakati wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama upya namna ya kufanya maboresho kwa mashindano ya vijana kwa kuwa hii ya Uhai tayari imeshafanyika hivyo itakuwa vizuri kama kutakuwa na mbadala wake.
Kuongeza mashindano mengine pia ambayo yatawahusu vijana yatafanya kuwe na chachu hasa kwa vijana kuweza kuimarika zaidi na kufanya timu zizidi kuwa na ushindani kwa kuwa muda mwingi zitakuwa kwenye mashindano.
Hebu pata picha kwamba kwa sasa vijana hawatakuwa na mashindano mengine watakuwa huru wakisubiri tena michuano ya Uhai msimu ujao, kwa kweli hapa kuna vingi ambavyo shirikisho linawafanya vijana wakae bila kujishughulisha hili sio jambo jema hasa kwa kukuza vipaji vyao hivyo mashindano yawe mengi zaidi.
Tuachane na hayo turudi kwenye mada ya leo hasa ambayo nimeamua kuizungumzia, wakati wa maendeleo ya soka ni sasa ambapo timu nyingi zinakwenda kusajili wachezaji na nyingine zinakwenda kuuza wachezaji.
Tayari vikumbo vimeshaanza kupigwa, saini zinasainiwa na wengine wanaondoka ni jambo jema kwa kuwa tayari dirisha limefunguliwa hivyo ni wakati wa kila timu kuhakikisha kwamba i n a k a m i l i sha usajili ili kuboresha zaidi timu.
Hivyo, napenda kutoa rai sasa kwa viongozi wa timu kufanyia kazi mapendekezo ya mwalimu na sio kufanya kazi kwa matakwa yao binafsi ama kwa mapenzi yao ili waweze kusajili mchezaji kwenye timu.
Jambo hili la uongozi kuingilia mamlaka ya mwalimu sio la kufumbia macho hata kidogo kwa kuwa anayefundisha ni mwalimu ndiye anayejua mahitaji ya timu yake na upungufu wa kikosi chake ulipo.
Hivyo suala la kila kiongozi ama uongozi wa timu kumpangia aina ya wachezaji halileti afya kwa timu kwa kuwa kufanya hivyo kutasababisha mwalimu awe na kazi ngumu katika kuhakikisha anakuwa na kikosi kizuri ambacho kitamsaidia kupata matokeo mazuri baadaye.
Timu inapopata matokeo mabaya uwanjani wa kwanza kubeba mzigo wa lawama ni mwalimu ambaye hakusikilizwa katika kufanya usajili sasa inakuwaje apewe mzigo ambao huenda angeweza kuupunguza wakati wa usajili kwa kusajili wachezaji ambao alikuwa na mahitaji nao?.
Jambo hili inabidi litiliwe mkazo na viongozi wote kwa kuhakikisha kwamba wanafanya usajili kwa kutumia ripoti ya mwalimu ambayo imekabidhiwa hivyo kuna umuhimu wa kufanya mambo kwa sasa kitaalamu zaidi.
Viongozi wenye wachezaji wao mkononi wanapaswa wazingatie ripoti ya mwalimu ina taka kitu gani kwa kuwa hakuna timu ambayo itafanya usajili bila kupitia ripoti, litakuwa jambo la ajabu sana hasa kuelekea kwenye ligi ambayo ina ushindani mkubwa sana.
Zama zimebadilika sana kwa sasa hivyo jambo la msingi ni mwalimu kusikilizwa mapendekezo yake ili kufanya kazi yake kwa uhuru hata itakapotokea amefanya vibaya aweze kujua namna ya kujipanga hasa kwa wachezaji ambao amewapendekeza hivyo atajua namna ya kuwatumia.