
BINGO! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mwanadada Wakonta Kapunda, kujipatia fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni hamsini na tano (55), kupitia mashindano ya mawazo ya biashara, yaliyoanzishwa na mfanyabiashara mkubwa nchini Dk. Regnald Mengi na fedha nyingine ni msaada toka kwa Rais Dk. John Magufuli.
Baada ya kushinda mashidano hayo yaliyokwenda kwa jina la Dream to Greatness, akiwa ni miongoni mwa washindi wawili kwani mshindi mwingine alikuwa ni Mr. Brian Mwenda kutoka Kenya, Dk. Mengi alimpa Wakonta, ambaye amepooza kuanzia mabegani hadi miguuni kutokana na tatizo la ‘spinal cord injury’, fedha taslimu dola 20,000 ambazo ni zaidi ya milioni 40 za Kitanzania.
Kama haitoshi Rais Magufuli ‘JPM’, alimzawadia milioni kumi za Kitanzania ndipo jumla zikawa zaidi shilingi milioni 55. Je, unafahamu fedha hizo Wakonta amepanga kuzifanyia nini? Ameeleza kila kitu pamoja na mambo mengine juu ya maisha yake kwenye makala haya ‘exclusive’. Huyu hapa akizungumza na Ijumaa;
IJUMAA: Hongera sana Wakonta kwa fedha ulizopata.
WAKONTA: Asante sana.
IJUMAA: Ulitegemea kwamba utashinda mashindano haya?
WAKONTA: Ndiyo, nilikuwa nina imani kubwa kwa sababu unapokwenda kushindana unachoamini ni kwamba wewe ndiye unastahili ushindi.
IJUMAA: Tayari umeshinda na fedha unazo, pengine umepanga kuzifanyia nini?
WAKONTA: Nimepanga kuzifanyia biashara. Lakini pia nipo katika hatua za kufungua ‘foundation’ yangu ambayo itakuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaoishi na tatizo kama langu la Spinal Cord Injury.
Juu ya yote ni kuboresha huduma yangu kwenye mitandao ya kijamii hasa YouTube, kwani nitaanza kuonyesha maisha yangu ya kila siku ili niweze kuwadhihirishia watu wanaoishi na tatizo hili wajione kwamba hawapo peke yao.

Lakini kuonyesha namna mtu mwenye tatizo hili anaweza kufurahia maisha, kuwa na uhusiano na hata kuwa na familia yake. Mategemeo ni kipindi hiki baadaye kuonekana kwenye kituo chochote cha televisheni.
IJUMAA: Umezungumzia kuhusu mtu mwenye tatizo lako kuwa kwenye uhusiano na kuwa na familia, vipi kwa upande wako?
WAKONTA: Bado sijawa na familia, lakini inawezekana kuwa na familia na uhusiano pia.
IJUMAA: Kuna kipindi ulikuwa unazungumzia kufanya muvi, mipango kwa sasa imefikia wapi?
WAKONTA: Mipango inaendelea, nilikwisha andika miswada mingi nipo najipanga ili tu watu waingie lokesheni na kuanza kushuti na mwaka huu ninategemea kuachia muvi moja.
IJUMAA: Umepanga kufanya na nani na itaitwaje?
WAKONTA: Nitafanya na wasanii ambao wengi ni rafiki zangu na jina bado hatujakubaliana, lakini wakati ukitimia nitalizungumzia hili.
IJUMAA: Kwa sasa upo wapi na maisha yako ya kawaida unayaendeshaje?
WAKONTA: Kwa sasa nipo nyumbani Mbeya. Ninaishi kwetu kwenye familia yetu ambayo ipo karibu sana na mimi. Ninajishughulisha na biashara pia, ikiwemo kumiliki duka la Wakeneji Shopping Mall.
WAKONTA ALIPATA TATIZO HILI LINI?
Ilikuwa ni Februari 2, 2012, majira ya saa nne na nusu asubuhi wakati wahitimu watarajiwa wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe mkoani Tanga wakiwa kwenye shangwe na shamrashamra kwenye sherehe ya kuagwa, kwani walikuwa wanaelekea kumaliza muda wao wa masomo shuleni hapo. Shangwe zikiwa zinaendelea, Wakonta akiwa miongoni mwa wasichana wenye furaha shuleni hapo, kishindo kikubwa kilisikika kwenye moja ya jengo la darasa, shuleni hapo.
Ilikuwa ni ajali mbaya iliyosababishwa na mmoja wa wahitimu ambaye aliingia kwenye gari la kaka yake aliyefika kumtembelea kwenye mahafari hayo na kuendesha huku akiwa hana ujuzi wowote.
Baada ya kukanyaga mafuta, gari lilichomoka kwa kasi na kwenda kuvaa ukuta, ajali mbaya ikatokea vifo kadhaa vikatokea na majeruhi akiwemo Wakonta wakapatikana. Hapo ndipo tatizo lake lilipoanzia.

Ni miaka sita sasa imepita lakini Wakonta mwenye miaka 26, ambaye anasema tatizo hili kidaktari halina tiba zaidi ya kutibiwa kwa dawa za asili, anaishi kwa furaha. Anajikubali kwa hali aliyonayo na anamshukuru Mungu kwa kila kitu.
Zaidi anamalizia kwa kusema: “Haijalishi ulivyo; uko mzuri, hauko peke yako na lolote ulitakalo linaweza kutimia ukiweka imani, juhudi na msisitizo wa kutosha. Unastahili vilivyo bora. Jipe vilivyo bora. Usipokee kimoja wala mmoja aliye chini ya ubora wako.”
MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE