JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema kwamba askari waliokuwa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Usafirisaji, NIT, Akwilina Akwilin walikwishaachiliwa huru kutokana na upelelezi kuonesha hawakuhusika.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa wakati akijibu swali la waandishi nwa habari waliotaka kujua nini kinachoendelea dhidi ya askari ambao waliwekwa rumande wakati wa upelelezi uliokuwa ukihusisha mauaji ya mwanafunzi huyo.
“Ni kweli askari walishikiliwa ili kufanyika uchunguzi katika mauaji yale, na mazingira ya kifo yalielezwa vizuri. Upelelezi ulionesha Askari hawakushiriki kwenye mauaji hayo ila kilichosababisha ni maandamano haramu ambayo yalisababisha watu kukusanyika vurugu zikatokea milipuko ya risasi ambayo ilipelekea tukio lile kutokea. Wale askari walitoka kutokana na jalada lilipopelekwa kwa mwanasheria ilionekana kuna udhaifu ndiyo maana hawajashtakiwa,” alisema Mambosasa.
Mbali na hayo, Kamanda Mambosasa ameongeza kwamba pamoja na kuwa inahisiwa askari ndiyo waliorusha risasi kwenda kwa waandamanaji, hisia hizo haziwezi kutengeneza kosa.
“Hisia hata ziwe nzito kiasi gani hazitengenezi kosa ninachosema ni matokeo ya upelelezi. Kesi iliyopo ni waandamanaji waliosababisha tukio kutokea. Viongozi waliokuwepo kwenye maandamano wote wana silaha ingawa hatujajua ni silaha ya nani ilitumika” ameongeza.
Akwilina aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji NIT aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 wakati Jeshi la Polisi likiwatawanywa waandamanaji wa CHADEMA, Kinondoni Jijini Dar waliokuwa wakielekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.
Hata hivyo kwa sasa viongozi wa juu wa CHADEMA pamoja na wabunge saba wa chama hicho kwa sasa wanakabiliwa na kesi Na. 112/2018 katika mahakama ya Kisutu ambapo moja ya mashtaka yanayowakabili ni kufanya maandamano haramu yaliyopelekea mauaji ya mwanafunzi Akwilina.