
MABINGWA wa Soka Tanzania, Simba wameonyesha wamepania kufanya kweli baada ya kuongeza nguvu ya benchi lake la ufundi.
Simba wamechukua kocha mwingine akiwa ni raia wa Tunisia aitwaye, Adel Zrane. Huyu ni kocha wa viungo ili kuimarisha fiziki ya kikosi.
Zrane anachukua nafasi ya kocha wa viungo wa Simba, Mohammed Habib ambaye aliondoka pamoja na aliyekuwa kocha mkuu, Pierre Lechantre.
Tayari Zrane ameanza kazi na Simba jana kwenye Viwanja vya Milima ya Kartepe hapa Uturuki.
Kocha huyo ameanza kazi akishirikiana na kocha mkuu mpya wa Simba, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji ambaye pia alianza kazi rasmi nchini Uturuki.
Simba ipo hapa Uturuki ambako imeweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine.