×

Kesi ya Mbowe, Wenzake Yaahirishwa Tena

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajiwa kuanza usikilizwaji wa awali Julai 31 mwaka huu wa shauri la kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  Freeman Mbowe na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka 13 likiwemo la kufanya mkusanyiko usio halali Februari mwaka jana.

 

Shauri hilo lilikuja leo mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa. Wakili wa serikali, Faraja Nchimbi, ameiambia mahakama kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa baada ya maombi ya washtakiwa waliyokuwa wameyawasilisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutupiliwa mbali na hivyo akaiomba mahakama kuendelea na usikilizwaji wa awali.

 

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili, Nashon Nkungu, umeieleza mahakama kuwa baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutupilia mbali maombi yao Julai 20 mwaka huu,  waliamua kukataa rufaa katika Mahakama ya Rufani ambapo bado wanasubiri maombi yao, hivyo akaiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokuendelea na usikilizwaji huo wa awali ambapo hakimu hakukubaliana na hoja hiyo kwani maombi yao yalitakiwa yawasilishwe mahakamani hapo kwa njia rasmi ya vielelezo vya baaua ya rufani.

 

Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Mbali na Freeman Mbowe, viongozi wengine wa Chadema katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa;  Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

 

Wabunge wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche;  Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

 

HABARI: DENIS MTIMA | GPL