×

SPIKA JOB NDUGAI MGENI RASMI SIMBA VS YANGA UWANJA WA TAIFA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) Limemtangaza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kuwa mgeni rasmi wa mchezo wa Ligi kuu Tanzania Bara (TPL) kati ya Simba na Yanga. Simba na Yanga zinakutana leo katika mchezo wa Ligi kuu kuanzia majira ya saa 11 jioni ukiwa ni mchezo uliosubiriwa kwa muda mrefu.

TFF wametoa taarifa hiyo kupitia mtandao wao wakimtangaza Mhe. Job Ndugai kuwa mgeni rasmi wa mechi hiyo ya watani wa jadi huku viongozi mbalimbali nao wakitarajia kuja kushuhudia mchezo huo.

Simba na Yanga zinakutana katika Ligi kuu Tanzania Bara ikiwa ni mara ya 93, Yanga akishinda mara 34 na Simba mara 26 huku wakitoka sare mara 30. Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini utakuwa wa kusisimua kwa kila upande kutaka kuibuka na ushindi.

Kwenye mchezo wa msimu timu hizo zilicheza jumla ya mechi tatu, Mbili zikiwa za Ligi ambapo Simba alifanikiwa kushinda mchezo moja kwa goli 1-0 likifungwa na Erasto Nyoni, mchezo mmoja wakitoka sare 1-1 magoli yakifungwa na Shiza Kichuya kwa upande wa Simba na Obrey Chirwa akisawazisha. Mchezo mwingine ni Ngao ya Jamii Simba wakishinda kwa mikwaju ya penati baada ya kumalizika kwa dakika 90.

Yanga waliokuwa wameweka kambi yao Mji kasoro bahari Morogoro na Simba hapahapa Jijini Dar es Salaam zitashuka dimbani kutafuta nani zaidi.