×

Mbelgiji wa Simba ampa onyo Chama

KOCHA Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems ameshindwa kuzuia hisia zake na kutamka kuwa timu yao imepata kiungo kwa Mzambia, Claytous Chama huku akimpa onyo kali.

 

Chama alijiunga na Simba kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Power Dynamo ya Zambia ambaye hadi hivi sasa tayari ametengeneza nafasi moja ya bao huku mwenyewe akifunga mawili dhidi ya Stand United na Alliance.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Aussems alisema Chama ni kati ya wachezaji wenye vipaji Afrika huku akiamini ni hazina kubwa kwa nchi yake ya Zambia kwa siku za baadaye.

 

Aussems alisema, kiungo huyo hatakiwi kubweteka na sifa nyingi anazoendelea kuzipata akiwa na Simba baada ya kuonyesha kiwango tangu ajiunge na timu hiyo.

“Huyu kijana ana kipaji cha hali ya juu. Ni hazina kubwa kwa nchi yake ya Zambia. Ninamshauri asibweteke, azidi kujituma, ni suala la muda kwake kwenda kucheza kimataifa.

 

“Ninaamini kama akiendelea kushikilia nidhamu yake nzuri aliyo nayo huku akifuata mafunzo na maelekezo yangu, basi namtabiria kufika mbali. Kikubwa ni kufuata miiko na maadili ya soka pekee, wachezaji wengi wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na nidhamu ndogo,” alisema Aussems.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam