×

Kwa Simba hii unakufa tu

SIMBA ya sasa ukikutana nayo unakufa tu, hakuna ubishi kuhusu hilo, jana imefanikiwa kushinda mechi ya nne mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Ni baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku mastraika Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wakiongoza mpango mzima wa mauaji. Baada ya kutoka sare na Yanga, Simba imeshinda mechi nne mfululizo dhidi ya Lyon, Stand, Alliance na Ruvu Shooting.

 

Lakini mastraika wa Simba wameonekana kuwa kiwembe zaidi, huku Emmanuel Okwi akirejea kwenye ubora wake kwa kufunga katika mechi nne mfululizo pia.

 

Jana Okwi alifunga mabao matatu ‘hat trick’ na kufikisha mabao saba katika mechi nne zilizopita, huku Simba ikifikisha mabao 21, ikiwa inaongoza kwa kufunga mabao mengi katika ligi nzima. Ukitaka kupatamabao ya Simba, utatakiwa kuchukua mabao 15 waliyofunga Yanga ujumlishe na mabao sita waliyofunga KMC, ama Lyon au Mwadui ambazo zote zina mabao sita.

 

Ushindi huo umeifanya Simba kuishusha Yanga na kupaa hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 23, wakati Yanga imebaki na pointi 22. Katika mchezo mwingine, Azam ikiwa ugenini iliichapa Singida United bao 1-0 kwenyeUwanja wa Namfua, huku bao hilo pekee likifungwa na Donald Ngoma.

 

Azam imefikisha pointi 27, ikiwa na michezo 11, wakati Simba ni wa pili wakiwa na michezo 10, kama wakishinda kiporo chao, watabakiza pointi moja tu kuwafikia Azam.

 

Katika mchezo wa mchana, JKT iliichapa Tanzania Prisons bao 1-0 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar. Mtibwa wenyewe walifanikiwa kuwachapa Kagera bao 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro huku Alliance na Coastal Union zikitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

 

Katika mchezo wa Simba, Okwi alianza kuifungia Simba bao la mapema dakika ya 7 tu, baada ya kuitendea haki krosi ya Shomari Kapombe na kumchambua kipa kasha kufunga. Kagere aliifungia Simba bao dakika ya 23, baada ya kumalizia mpira wa kichwa uliopigwa na John Bocco uliogonga mwamba na kurejea uwanjani.

 

Hata hivyo, dakika ya 35, Kagere alianguka chini baada ya kugongana na mchezaji wa Ruvu Shooting, na alitolewa nje kwa machela lakini alirejea uwanjani dakika ya 39.

 

Okwi alirudi tena kambani dakika ya 52, baada ya kumalizia krosi safi iliyopigwa na Kapombe, Okwi alifunga tena dk ya 77 kwa pasi ya John Bocco, na sasa amepanda hadi nafasi ya kwanza kwenye chati ya wafungaji akiwa na mabao 7, sawa na Eliud Ambokile wa Mbeya.

 

Okwi alitolewa uwanjani dk ya 84 baada ya kuumia goti na nafasi yake ikachukuliwa na Adam Salamba ambaye alifunga bao la tano dk ya 88. Akizungumza na gazeti hili juzi, Okwi alisema siri ya mabao yake ni kuelewana na wenzake kwenye eneo la ushambuliaji.

 

“Kwa sasa tumeanza kuelewana, ndiyo maana unaona mimi nafunga, lakini tunapata ushindi kwenye mechi zetu, lakini bado tuna kazi ya kufanya kwa sababu kuna nafasi tunashindwa kuzitumia vizuri,” alisema Okwi.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

OKWI Alivyokabidhiwa Mpira Baada ya Kupiga Hat Trick