
Nyota wa muziki wa pop na mbunge wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu amekataliwa kufanya tamasha lake leo Disemba 26 kama alivyokuwa amepanga hapo awali.
Msemaji wa polisi nchini Uganda, Emilian Kayima amesema kwamba Bobi Wine alikuwa hajaandika barua ya kuomba ruhusa kufanya tamasha hilo ndio maana hawawezi kumruhusu.
“Tutakuwa katika ufukwe wa Busabala kuzuia shughuli hiyo na kuhakikisha usalama upo.Tamasha hili halikuwa limeruhusiwa kufanyika kwa sababu ya kutokidhi vigezo”, Kayimba alisema.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda limeeleza kwamba mapema leo, Bobi Wine aliandika kwenye mtandao wa kijamii kuwa kikosi cha usalama kimevamia tamasha lake la ‘One Love Beach in Busabala’ na kuwakamata wafanyakazi wake
Hili lingekuwa tamasha la pili la Bobi Wine kufanyika, tangu ashtakiwe na kufungwa kwa mshtaka ya uhaini.
