×

GLOBAL HABARI JAN 05: Waziri Mkuu Acharuka, Apiga Marufuku Kahawa Kusafirishwa! – VIDEO

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA ametoa agizo la kuzuia mauzo ya kahawa isiyokobolewa nje ya nchi ili kuongeza mnyororo wa thamani na kusaidia kulinda uwekezaji wa viwanda unaofanyika nchini.

Waziri mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa kahawa wa mkoa wa Ruvuma na kusisitiza kuwa kahawa yote itakayozalishwa nchini ni lazima iongezewe thamani na hakuna kahawa yenye maganda itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa agizo la kuigawa minada ya kahawa nchini katika kanda maalumu ambazo zitarahisisha mauzo ya kahawa pamoja na bei kufahamika kwa wakati, huku akiwaagiza viongozi wa vyama vya ushirika vinavyosimamia uuzaji wa mazao ,AMCOS, kuhakikisha wakulima wote wanasajiliwa ili wanufaike na kazi wanazofanya.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Serikali kusimamia zao la kahawa kwa ukaribu na kupongeza utaratibu wa kugawa minada ya kahawa katika kanda maalumu.

Hata hivyo waziri mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haitorudi nyuma katika msimamo wake wa kuwasimamia wakulima nchini ili nao waweze kunufaika na kazi kubwa wanazofanya.