×

SZIFF ILIVYOWALIZA MASTAA BONGO

RICHARD BUKOS

USIKU wa kuamkia juzi (Jumapili) Jiji la Dar es Salaam lilisimama kwa muda kushuhudia sherehe za utoaji wa Tuzo za Filamu za Kimataifa zijulikanazo kama Sinema ZetuSZIFF’ ambapo pia ziliacha mastaa wengi wakilia kubwagwa na wasanii chipukizi kitendo ambacho hawakukitarajia.

 

VIONGOZI KAMA WOTEE

Katika sherehe hizo zilizofanyika ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City zilikusanya watu maarufu pamoja na viongozi akiwemo, mgeni rasmi Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Ali Abeid Aman Karume, pamoja na Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shigongo.

 

 

RUBY ASIMAMISHA UKUMBI

Shangwe za kutosha ziliibuka baada ya mwanadada, Hellen George ‘Ruby’ kupanda jukwaani na kuusimamisha ukumbi kwa muda huku akitunzwa noti za shilingi elfu kumi kama zoteee ambazo zilimuogeshwa mwili wake.

Baada ya burudani hiyo tukio la utoaji wa tuzo liliendelea kutikisa kwa vipengele mbalimbali vilivyokuwa vikiwaniwa ikiwemo waigizaji, watayarishaji miswada, watengeneza makala, waandishi wa filamu fupi na ndefu waongozaji pamoja na vinginevyo.

Msanii mwingine wa Bongo Fleva, Mbosso kutoka Wasafi Classic Baby ‘WCB’ naye aliwapagawisha mashabiki kwa kuingia na madansa wa kike na wa kiume ambao wote walivalia nguo nyeupe.

 

 

MAAJABU YA TUZO TATU

Katika vipengele hivyo mastaa wengi wa filamu za kibongo walishirikishwa lakini mwisho wa siku wengi waliambulia patupu huku wasanii chipukizi wakijizolea tuzo wengine hadi tatu kwa mpigo.

Miongoni mwa wasanii chipukizi aliyefanya maajabu ukumbini hapo ni Christina Pande aliyejizolea tuzo tatu kwa filamu yake ya Supa Mama.

 

Katika filamu hiyo, Christina alitwaa Tuzo ya Mwandishi Bora wa Muswada, Mwandishi Bora wa Filamu Fupi na ya tatu ni Muandaaji Bora wa Filamu.

Christina aliliambia Over Weekend kuwa, filamu hiyo imeshampatia tuzo tano nje ya nchi na kuzitaja nchi hizo kuwa ni Nigeria, India, Rwanda, Burundi na Zanzibar na pia ilishirikishwa kwenye nchi nyingine kumi ambazo haikushinda.

 

WATOTO WAIBUA GUMZO

Katika muendelezo wa wasanii chipukizi kuwaliza wakongwe ni pale tuzo ya Msanii Bora wa Kike kuchukuliwa na mtoto anayelelewa na Kituo cha TAG Ismani cha Iringa, Flora Kiondo kutoka Kundi la Kesho kupitia filamu inayoitwa Kesho.

Baada ya kutangazwa mshindi huyo mastaa walitega sikio kusikilizia tuzo ya Msanii Bora wa Kiume ambapo napo ilikwenda kwa mtoto mwingine wa kundi hilohilo, Rashidi Msigalla kupitia filamu hiyo hiyo inayoitwa Kesho.

 

GABO CHUPUCHUPU

Msanii Gabo Zigamba ambaye wengi waliona huenda akachukua tuzo zaidi ya mbili kama alivyofanya msimu wa kwanza wa tuzo hizo, alibaki kuambulia moja tu na kunusurika kukosa kabisa.

HEMED ATOA YA MOYONI

Hemed Suleiman ‘PHD’ kutoka Bongo Movie aliyekuwa akiwania kipengele cha Msanii Bora wa Kiume alisema mchakato huo ameuona umeenda kwa haki na kuwapongeza waliojitwalia na kuwataka wakongwe wazidi kujipanga.

Msanii mwingine aliyezungumza na Over Ze Weekend ni Kulwa Kikumba ‘Dude’ ambaye alisema tuzo zimeshakwenda kwa wasanii wengi wasio na majina makubwa cha msingi ni wao kujipanga upya msimu ujao.

Mastaa wengine waliokuwepo ni Suzan Lewis ‘Natasha’ mwanaye, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ Wema Sepetu, Hamisa Mobeto, Elizabeth Michael ambaye alikuwa mshereheshaji ‘MC’, Tino, Esha Buheti, Kupa, Rammy Gallis, Miss Tanzania, Queen Elizabeth, Mpoki, Joti na wengine kibao.

 

MASTAA WALIOONESHA KULIA

Miongoni mwa mastaa walioonesha kulia kwa kubwagwa na wasanii wachanga ni pamoja na Wema Sepetu ambaye amesikika akisema kuwa ameumia lakini anajipanga upya.

Naye Johari alisema kuwa kuwapa wasanii chipkizi na kuwaacha wasanii wakubwa ni kuua sanaa hivyo aliwashauri waandaaji wangekuwa na kipengere cha msanii chipkizi na si kuwachanganya kitendo ambacho alionesha wazi hakufurahishwa nacho.

EXCLUSIVE: Watoto Walioshinda Tuzo ya Waigizaji Bora Wamfungukia Wema na Gabo