
WANAHARAKATI kutoka vyuo vikuu nchini, kupitia kampeni ya Wekeza Kwangu, wanatarajia kufanya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wasichana walemavu kutimiza ndoto zao.
Harembee hiyo inatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi katika kituo cha kuoshea magari cha Texas Bay Wash kilichopo jirani na Rose Garden, Mikocheni B jijini Dar, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuepukana na unyanyapaa kwa walemavu.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, mwenyekiti wa wanaharakati hao, Marilyn Mbogo, alisema kuwa katika harambee hiyo wataosha magari ya watu mbalimbali na fedha watakazolipwa zitatumika kuwasaidia wasichana walemavu.
“Kiukweli tumeamua kuanza na kundi la wasichana wenye ulemavu kwa sababu hawa wanapata wakati mgumu zaidi kutokana na nafasi yao, wana mahitaji mengi ya msingi, kama taulo za kike, fimbo kwa ajili ya wasioona, vifaa vya kusaidia usikivu (hearing aid) na mafuta ya kuzuia miale ya jua kwa wenye ulemavu wa ngozi.
“Mahitaji ni mengi lakini tutaanza na machache kutegemea na hamasa itakavyokuwa kwa watu ambao watajitokeza kesho. Tutaosha magari kwa bei ya shilingi 15,000 lakini hata kwa walio mbali, wanaweza kuchangia kwenye akaunti yetu kupitia Benki ya CRDB, 015041659700 au kwa Tigopesa namba 0658 689 848,” alisema Mbogo.




