
UNAPOTAJA washambuliaji wazawa ambao wapo kwenye kasi ya hatari ya kupachika mabao basi kamwe huwezi kuliweka kando jina la John Bocco.
Bocco ambaye hivi karibuni mabosi wa Simba walimuongezea mkataba wa kusalia klabuni hapo kwa misimu miwili zaidi anabaki kama kielelezo cha washambuliaji wazawa ambao wanajua kufunga kutokana na takwimu zake.
Amefunga zaidi ya mabao 100 kwenye Ligi Kuu Bara lakini pia ndani ya misimu miwili iliyopita amefunga zaidi ya mabao 30.
Championi Jumatano, limefanya makala na straika huyo na hapa anafunguka kama ifuatavyo.

UMEJIPANGAJE KWA MSIMU UJAO? “Mimi niko vizuri na nimejiandaa kuipambania klabu yangu kwa msimu
ujao baada ya msimu ulioisha kumalizika. Kitu kikubwa ninataka kujitoa zaidi ya vile ambavyo nilifanya msimu ulioisha.
MLIFANYA VIZURI MSIMU ULIOPITA, MSIMU UJAO TUTARAJIE NINI?
“Kwanza kwa sasa tunajiandaa na msimu mpya wa ligi na tunaendelea na kambi yetu. Tumesahau juu ya kila kitu ambacho tulikifanya kwa msimu uliopita na sasa tunachoangalia ni juu ya msimu huu. “Tunajua tunatakiwa kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita na tunajipanga kwa ajili ya hilo.
UNAWAZUNGUMZIAJE WACHEZAJI WAPYA WALIOSAJILIWA?
“Kwanza tunawakaribisha wachezaji wote waliokuja msimu huu. Sisi hapa Simba tuna umoja sana naamini tutashirikiana nao vizuri. “Katika usajili wao nadhani waalimu waliona mapungufu yetu wapi tulikuwa tunakosea ndiyo maana wakawasajili wao, naamini wachezaji waliokuja watakuja kutubusti na kupata mafanikio. “Nawakaribisha na tutawasapoti kama wachezaji kwa ajili ya kufanya vizuri.
KUNA TOFAUTI GANI YA KAMBI YA AFRIKA KUSINI NA ILE YA UTURUKI?
“Ndiyo tulienda Uturuki kujiandaa na msimu uliopita na sasa tupo hapa Sauz, mimi nina choona ni kwamba viongozi na benchi la ufundi wao ndiyo wana zingatia ni wapi tukaweke kambi. Hakuna tofauti kubwa kwani kambi ni kambi tu.
MSIMU UJAO UTAMKOSA OKWI, UNAFIKIRI LITAKUWA PIGO?
“Hilo la Okwi sitaki kulizungumzia sana kwa sababu ni suala la benchi la ufundi na viongozi, mimi nadili na masuala ya kiuchezaji tu. Lakini naamini wachezaji waliopo tutafanya vizuri tu.
MTAFIKA TENA ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA?
“Hiyo ni ndoto yetu kuona kwamba tunapambana kutimiza vile tulivyofanya kwa msimu uliopita. Tunataka kufi ka mbali zaidi kwa msimu huu kwenye michuano hiyo.
USAJILI HUU ULIOFANYWA UNAUONAJE?
“Ni mzuri kila mchezaji ambaye amekuja hapa ni mzuri na ataipigania timu. Benchi la ufundi na viongozi wamesajili watu wazuri ambao ninavyoona watatusaidia sana kwa msimu ujao wa ligi na michuano mingine.
NINI MNAWAAHIDI MASHABIKI WENU?
“Ni kimoja tu. Tutapambana zaidi kama wachezaji kuliko msimu uliopita ili kupata matokeo mazuri kwenye kila mechi yetu ambayo tutacheza. Nafi kiri hilo ndiyo jambo pekee wasubirie kuliona.
UMEPANGA KUFUNGA MABAO MANGAPI?
“Siwezi kuweka idadi maalum kwamba nitafunga hapo tu lakini nitafunga kila mara ambapo nitapata nafasi ya kufanya hivyo. Lakini hata ikitokea sitafunga basi niweze kuwa sehemu ya ushindi kwa kikosi changu.
UNAONA ITAKUWA RAHISI KUTETEA UBINGWA?
“Hapana haitakuwa hivyo kwa sababu kila timu imejipanga kushindana, hivyo ni juhudi zetu kuhakikisha tunajitolea zaidi ili mwisho wa msimu tena tutetee ubingwa wetu kwa mara nyingine zaidi.
MMEJIWEKEA MALENGO GANI?
“Kitu kikubwa tunaenda kuwasikiliza makocha na viongozi kile wanachokitaka na kuangalia kila kitu ambacho watakuwa wanakitaka. Kwa umoja wetu basi kila kitu kitaenda sawa,” anamaliza Bocco.