
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, aliyetupia tatu dhidi ya Moro Academy juzi, Patrick Sibomana, amewaambia mashabiki kwamba ndiyo zake wala hakubahatisha wazisubiri nyingi Uwanja wa Taifa.
Amesisitiza kwamba, hata Township Rollers lazima wawapige si chini mabao matatu na kuendelea pale Taifa ili kuthibitisha kwamba wamerudi vizuri kimataifa.
Yanga ambao imefanya usajili wa aina yake msimu huu, itacheza na timu hiyo kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Kocha Mwinyi Zahera akitarajiwa kutua Dar es salaam leo Alhamisi akitokea kwao Ufaransa na kupitiliza moja kwa moja Morogoro.

Township ipo kambini Afrika Kusini na Yanga imejikita Morogoro. Katika ratiba hiyo, Yanga itaanzia nyumbani kucheza na Township Rollers ya Botswana kati ya Agosti 9 hadi 11, mwaka huu na kurudiana ugenini Agosti 23 hadi 25, mwaka huu.
Sibomana aliyejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea Mukura Victory ya kwao Rwanda, amesema lazima washinde mchezo huo wa nyumbani kwa ushindi mnono ili wakienda ugenini kazi iwe rahisi.
“Tunaanzia nyumbani, ni kitu kizuri kwani mechi za nyumbani ni nzuri kuanza na ushindi, mkienda ugenini na ushindi, basi mnawapa shida wapinzani wenu.

“Katika mchezo huo, lazima tushinde kuanzia mabao matatu ili iwe kazi kwao kusawazisha kwani nawafahamu sana. Wale ni watu wenye fitina sana wakiwa nyumbani kwao,” alisema sibomana ambaye anafanya vizuri kwenye mazoezi yanayoendelea mjini Morogoro.
MSIKIE BIGIRIMANA straika mpya, Issa Bigirimana
raia wa Rwanda, amesema ; “Tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo na Township Rollers, hii ni kazi yetu na lazima tuipambanie timu kuhakikisha kwamba inafanya vizuri katika mechi hiyo.”
Kwa mujibu wa uongozi wa Yanga, Zahera anajua kila kitu kilichokuwa kinaendelea kambini kwani ndiye aliyekuwa akiratibu na kwamba leo akishatua atakaa kikao kizito na wachezaji ambao wengi hajaonana nao tangu aidhinishe usajili wao. Zahera amepanga kuwaambia wachezaji hao malengo yake na utaratibu wake wa kazi kitaifa na kimataifa.
MUSA MATEJA NA SAID ALLY