
KOCHA wa Zesco ya hapa, George Lwandamina amemsainisha kiungo fundi aliyetemwa na Yanga, Thabani Michael Kamusoko kwa dili la miaka mitatu. Lwandamina aliwahi kuikochi Yanga na kuingia mitini kiaina.
Timu hiyo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo kama hesabu zao zikienda vizuri kuna uwezekano wa kukutana kwenye raundi ya kwanza mwezi ujao.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zesco, Richard Mulenga ameliambia spoti Xtra kwamba, wamemsainisha mchezaji huyo kwavile benchi la ufundi linaujua uwezo wake.
“Tunaijua kazi yake, tunategemea kazi nzuri kutoka kwake,” alisema Mulenga akimzungumzia Kamusoko ambaye Yanga waliwahi kumpachika jina la Kampa Kampa Tena enzi hizo alipotua akitokea Platinum ya Zimbabwe. Yanga wamemtema mchezaji huyo ambaye mkataba wake umemalizika kwa madai kwamba kiwango chake kimechuja.