
KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera ametua nchini juzi usiku na kimyakimya uongozi ukaenda kumpokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA) jijini Dar es Salaam na kumficha hotelini kabla ya hivi karibuni kumsafirisha kwenda Morogoro kujiunga na kambi ya timu hiyo.
Awali, kocha huyo mwenye uraia wa Ufaransa na DR Congo alitarajiwa atue nchini tangu Jumatatu iliyopita kabla ya juzi kutua nchini akitokea nyumbani kwake Ufaransa ilipo familia yake.
Kocha huyo kwa mara ya kwanza atakiona kikosi chake kipya kikicheza mchezo wake wa nne wa kimataifa dhidi ya Mawenzi Market utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kocha huyo alitua nchini juzi asubuhi na kupokewa na viongozi wa timu hiyo na kuomba kupumzika baada ya uchovu wa safari na jana alfajiri alielekea Morogoro kujiunga na kambi hiyo.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa mara baada ya kutua nchini alitarajiwa kukabidhiwa gari jipya la kisasa aina ya Toyota Crown Athlete lenye thamani ya Sh milioni 15 ambalo atatembelea hivi sasa na siyo Toyota Brevis tena.
Aliongeza kuwa kocha huyo baada ya kuwasili nchini alieleza sababu ya kuchelewa kujiunga na timu hiyo huko baadhi ya vigogo wa timu hiyo wakihusika kwa kumpigia simu kumzuia kujiunga na kambi yake huko Morogoro. “Yapo mambo mengi yanayoendelea hivi sasa katika timu na hayo ni baada ya moja ya kampuni kushindwa katika tenda ya jezi iliyotolewa na viongozi wapya walioingia madarakani.
“Watu hao ndiyo walichelewesha ujio wa Zahera baada ya kumpigia simu na kumzuia asije nchini hadi watakapomlipa stahiki zake zote kabla ya viongozi kumpigia simu na kueleza hayo yote na baadaye kumshawishi na kukubali kurejea kujiunga na timu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Championi Jumatatu limeelezwa kuwa watu hao wanataka kuona Yanga inafanya vibaya ili uongozi uonekane haufai, kwa kuwa tu walinyimwa tenda ya jezi.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo, alisema: “Kocha yupo safari hivi sasa, anaelekea Morogoro baada ya kutua nchini akitokea Ufaransa.
“Na leo (jana) huenda akakaa benchi katika mchezo wetu wa kirafiki dhidi ya Mawenzi Market, hivyo mashabiki wawe watulivu katika kipindi hiki tukielekea katika kilele cha Wiki ya Mwananchi.”